Mawakili wa Nairobi waipa JSC siku 14 kumchunguza jaji Chitembwe, watishia kumfukuza

Muhtasari
  • Mawakili wa Nairobi waipa JSC siku 14 kumchunguza Chitembwe, watishia kumfukuza 
Mawakili wa Nairobi waipa JSC siku 14 kumchunguza Chitembwe, watishia kumfukuza 
Image: Andrew Kasuku

HABARI NA ANNETTE WAMBULWA;

Mwenyekiti wa LSK Nairobi Eric Theuri ameipa Tume ya Huduma ya Mahakama siku 14 kumchunguza Jaji Said Chitembwe, ambapo mawakili wote wa Nairobi watamuondoa ofisini kwa nguvu.

Theuri alikuwa akijibu video iliyowekwa mtandaoni na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko akidaiwa kumuonyesha jaji akijadili jinsi ya kuafikiana na kesi.

Pia ametishia kuwa mawakili watasusia mahakama ya jaji Chitembwe ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa dhidi yake.

Theuri amemshauri hakimu 'kutafuta nafsi' na kuchunguza dira yake ya maadili na ikiwa madai hayo ni ya kweli anapaswa kung'atuka.

Chitembwe alikuwa mmoja wa majaji wawili waliokamatwa mwezi Julai baada ya polisi kusema walipata taarifa kuwa walikuwa na nia ya kupokea hongo.

Baadaye aliambia mahakama mwezi Septemba kwamba kupatikana na dola si jambo la kawaida kwani familia yake inaendesha akaunti ya fedha za kigeni.

Chitembwe alishangaa ni kwa nini polisi walimshuku kwa ulaghai walipompata akiwa na dola 7,000 mfukoni alipokamatwa pamoja na Jaji Aggrey Muchelule mnamo Julai.

Lakini Chitembwe, katika hati ya kiapo iliyowasilishwa katika Mahakama ya Juu kupitia kampuni ya mawakili ya Otieno Okeyo, alikanusha kuhusika na ulaghai, akisema kupatikana na dola hapaswi kushukiwa.

Zaidi ya hayo alieleza kuwa dola husika zilikuwa mfukoni mwake na kwa hiari yake alizisalimisha kwa polisi ingawa alikusudia kutumia pesa hizo kulipia karo ya shule ya mwanawe.

Kulingana na hati hiyo ya kiapo, baada ya upekuzi katika vyumba vyake Julai 22, alitoa dola 7,000 kutoka mfukoni mwake "kwa ajili ya ada ya shule ya mwanangu katika Chuo Kikuu cha Edith Cowan, Perth Australia", ambayo alikabidhi kwa polisi.