Mwanamume akamatwa kwa kutishia kumuua mwingine, kumkata vipande vidogo

Muhtasari
  • Mwanaume akamatwa kwa kutishia kumuua mwingine, kumkata vipande vidogo
Amar Dilip Shah,
Image: DCI/Twitter

Mwanamume mmoja mwenye asili ya Kihindi mwenye makazi yake Nairobi alikamatwa Ijumaa na DCI kwa madai ya kutishia kumuua mtu mwingine na kumkatakata vipande vidogo.

Mshukiwa huyo, aliyetambulika kama Amar Dilip Shah, alinaswa kando ya mtaa wa General Mathenge huko Westlands.

Kulingana na ripoti za polisi, Shah alisababisha kizaazaa kwa kujaribu kupinga kukamatwa na kumshambulia mpelelezi aliyemkamata lakini alishindwa.

“Kilichofuata ni kizaazaa huku mshukiwa mbovu akijaribu kumrushia mateke na ngumi Inspekta wa Polisi. Lakini afisa huyo ambaye pia ni mtaalamu wa sanaa ya kijeshi alimtiisha mwanamume huyo bila juhudi,” Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema katika taarifa.

Kwa sasa Shah anazuiliwa chini ya ulinzi halali wa polisi akisubiri kufikishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka ya kutishia kuua.

“Kukataa kukamatwa au kumshambulia afisa wa polisi, akitekeleza wajibu wake, kunavutia faini isiyozidi Ksh.1 milioni au kifungo kisichozidi miaka kumi au vyote kwa pamoja,” DCI alionya.