Fahamu athari za vita nchini Ukraine kwa uchumi wa Afrika

Muhtasari

• Mzozo wa kivita kati ya Urusi naUkraine unazidi kulemaza uchumi si tu barani Ulaya bali mpaka mataifa ya Afrika ambayo yako mbali sana na Ulaya.

• Mzozo huo umeathiri bei ya bidhaa mbalimbali kama gesi, mbolea, ngano miongoni mwa bidhaa zingine zinazotumika kwa sana haswa nchini Kenya.

Image: EPA

Vita kati ya Urusi na Ukraine vinazidi kulemaza na kuathiri shughuli nyingi za kiuchumi si tu barani Uropa bali hadi bara la Afrika, mfano nchini Kenya tayari athari za mzozo huo zimeanza kuonekana katika sekta mbalimbali.

Athari hizo zimeanza kushuhudiwa haswa katika sekta za mafuta na gesi ambapo bei za bidhaa hizo zimetajwa kupanda mara dufu, wiki mbili tu baada ya Urusi kuivamia Ukraine.

Katika kipindi hicho, bei ya mafuta ya kupika imezidi kupanda kwa kasi za duma, licha ya kwamba hapo awali imekuwa ikipanda lakini si kwa kasi kama hii ya sasa ambapo inasemekana taifa la Ukraine ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta ya kupika kote duniani.

Wachananuzi wa biashara za kimataifa wanasema kwamba bei ya gesi ambayo tayari iko kileleni huenda ikazidi kupanda zaidi kutokana na hali kuzidi kuwa tete nchini Ukraine ambapo wanajeshi wa urusi wameivamia na kuharibu mitambo mbalimbali ya kuzalisha bidhaa kama hizo.

Taifa la Urusi ni la tatu kati ya mataifa yanayozalisha gesi kwa wingi na inasemekana kutokana na mzozo wa vita na vikwazo ambavyo taifa hilo limewekewa na mataifa mengi barani Ulaya, huenda Urusi ikasitisha uuzaji na usambazaji wa gesi nje ya nchi hiyo na hivyo kusababisha uhaba kote duniani hatua ambayo itaathiri bei ya bidhaa hiyo hadi humu nchini.

Bidhaa nyingine ambazo Kenya na mataifa mengi ya Afrika hutegemea kutoka Urusi ni na Ukraine ni ngano ambapo katika takwimu za 2020, Kenya iliagiza ngano ya shilingi bilioni 16 kutoka Urusi.

Mbolea pia imekuwa ikipanda huku wakulima walizidi kulilia gharama kubwa hiyo ambayo wameitaja imepanda kwa kiwango cha mara tatu zaidi ya kiwango walichokuwa wakiinunua. Kupanda kwa bei hii kulihusishwa na vitisho vya mapigano baina ya mataifa hayo mawili kabla ya vita venyewe. Kupanda huku kwa bei ya mbolea kunamaanisha kwamba mwaka ujao bei ya vyakula sokoni itakuwa juu mno ikilinganishwa na mwaka huu.

Kwa mfano kenya haitaathirika kutoka kwa uagizaji tu bali pia hata kusambaza na kuuza bidhaa zake katika mataifa ya mashariki mwa Uropa. Itakumbukwa Kenya husambaza bidhaa za matunda kama parachichi na maembe katika mataifa ya Urusi na Ukraine ambayo pia ni miongoni mwa masoko makubwa ya majani chai na maua kutoka humu nchini.