logo

NOW ON AIR

Listen in Live

NCIC kuchapisha maneno yaliyopigwa marufuku katika kampeni za kisiasa

Kutokana na hali hiyo, majukwaa 36 ya mitandao ya kijamii yanafuatiliwa kwa karibu na tume hiyo.

image
na Radio Jambo

Makala18 March 2022 - 20:06

Muhtasari


  • Kutokana na hali hiyo, majukwaa 36 ya mitandao ya kijamii yanafuatiliwa kwa karibu na tume hiyo

Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano imepanga kuchapisha orodha ya maneno ya Kiswahili, Kiingereza na lugha za kienyeji ambayo yatajumuisha matamshi ya chuki yaliyowekwa kificho.

Mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia alisema maneno hayo yatapigwa marufuku kuanzia sasa katika mikutano ya hadhara, machapisho ya mitandao ya kijamii na vipindi vya mazungumzo ya kisiasa.

Kobia alizungumza Ijumaa wakati wa mkutano na wanahabari ofisini kwake.

"Hii itasaidia pakubwa katika kudhibiti matamshi ya chuki na kuhakikisha taifa letu liko salama wakati huu wa kuandaa uchaguzi," alisema.

Mkakati huo unakuja baada ya dhoruba kutokana na matumizi ya neno 'madoadoa' katika mikutano ya hadhara.

Neno hilo linachukuliwa kuwa na uwezo wa kuibua mivutano ya kikabila kabla ya uchaguzi wa Agosti.

Kinara wa ODM Raila Odinga na Seneta wa Meru Mithika Linturi wamejikuta wakizozana na NCIC kuhusu matumizi ya neno hilo.

Raila alitumia neno hilo Machi 9 alipopeleka kampeni zake za Azimio la Umoja hadi kaunti ya Wajir huku akipigia debe azma yake ya kuwania urais.

Kobia alisema mitandao ya kijamii inatumiwa zaidi na miungano ya Azimio na Kenya Kwanza kueneza matamshi ya chuki.

Kutokana na hali hiyo, majukwaa 36 ya mitandao ya kijamii yanafuatiliwa kwa karibu na tume hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema watakaopatikana na hatia wataondolewa na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya.

Kobia pia alisema timu za usalama zinapaswa kuwa macho na kukabiliana na wahalifu wanaosababisha migogoro baina ya jamii, inayosababishwa na wizi wa mali na uchochezi.

“Tunafahamu lengo la maovu kama haya ni kusababisha watu kuhama kutoka ndani. NCIC inasalia kujitolea kusuluhisha vizuizi vya barabarani kwa amani,” akasema.

Mwenyekiti huyo alisema uchoraji wa ramani ya maeneo yenye migogoro katika mikoa minane (mikoa ya zamani ya utawala) na NCIC unaendelea.

Alisema wametambua kaunti zaidi kwa uwezekano wa ghasia za kisiasa Kaskazini-mashariki na Pwani.

NCIC pia ilisema imegundua ongezeko la wizi wa mifugo, ambao wanadai ni kichocheo cha mvutano na migogoro kati ya jamii zinazoishi kando ya maeneo ya mipakani.

Pia ilisema inafuatilia kwa karibu maeneo motomoto katika kaunti za Kisumu, Kericho na Nandi.

 

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved