Wahuni waliotushambulia walikodishwa kuniua-Raila Odinga

Muhtasari
  • Alisimulia kuwa shambulio hilo lilikuwa baya na waliokolewa na maafisa wa polisi
Kinara wa ODM Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Kiongozi wa ODM Raila Odinga alilalamika kuwa kulikuwa na mipango ya kumuua yeye na timu yake baada ya mazishi ya Mzee Jackson Kibor huko Uasin Gishu.

Akizungumza Jumapili mjini Washington DC, Raila alisema kipindi cha kampeni kimekuwa cha amani isipokuwa kisa ambapo wahuni walikodiwa kuwaua.

"Baadhi ya wahuni waliajiriwa na walitaka kutuua," alisema.

Alisimulia kuwa shambulio hilo lilikuwa baya na waliokolewa na maafisa wa polisi.

"Uliona walichokifanya kwa chopa yetu," aliongeza.

Katika kisa hicho, kikundi cha vijana waliokuwa na ghasia walianza kurushia ndege yake mawe walipowasili kwa ajili ya mazishi ya Mzee Kibor.

Raila  alisema walibadili kidogo muda wa kuwasili na hilo ndilo lililowaokoa.

"Majambazi walikuwa na mipango, walijua tutafika saa ngapi na aina ya usafiri tuliopanga kutumia," alisema.

Zaidi ya hayo, Raila alisema kuwa Wakenya wanatarajia kuwa na kipindi cha kampeni za amani na uchaguzi wa amani utafanyika Agosti 9.

"Hadi sasa mambo yamesonga vizuri hadi hapa tulipo," aliongeza.

Raila kwa sasa yuko katika ziara ya wiki moja Marekani.

Anatarajiwa kukutana na makampuni makubwa ya teknolojia huko Silicon Valley, San Francisco, akiwa na maono ya kukuza uhusiano wa teknolojia kati ya Kenya na Marekani ikiwa atachaguliwa mwezi Agosti.

Siku ya Jumatatu, anatarajiwa kufanya mikutano na wachezaji muhimu kutoka Corporate America.

Raila ameandamana na magavana watatu, wabunge saba na viongozi wengi wa Azimio.

Wao ni pamoja na; Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi, Wabunge Richard Tongi (Nyaribari Chache), Memusi Kanchory (Kajiado ya Kati), na Esther Passaris (Mwakilishi wa Wanawake Nairobi).