Sababu ya kugura muungano wa Azimio-Alfred Mutua amwaya mtama

Muhtasari
  • Kulingana na Mutua, Azimio la Umoja lilipendelea tu baadhi ya vyama vya kisiasa, na kuacha vingine kama MCC gizani
Gavana wa Machakos Alfred Mutua wakati wa uzinduzi wa manifesto yake ya Urais katika hoteli ya Panafric, Nairobi mnamo Desemba 5, 2021.
Gavana wa Machakos Alfred Mutua wakati wa uzinduzi wa manifesto yake ya Urais katika hoteli ya Panafric, Nairobi mnamo Desemba 5, 2021.
Image: ISAIAH LANGAT

Gavana Alfred Mutua ameeleza ni kwa nini amegura muungano wa Azimio la Umoja na kujiunga na Muungano wa Kenya Kwanza Alliance mnamo Jumatatu.

Kulingana na Mutua, Azimio la Umoja lilipendelea tu baadhi ya vyama vya kisiasa, na kuacha vingine kama MCC gizani.

"Kwa ajili hiyo, tumeamua kuvunja uhusiano wetu na Azimio la Umoja. Kwa hiyo, mkataba kati ya Azimio na MCC ni batili."

Mutua anasema chama cha MCC kimefichwa katika maswala ya Azimio la Umoja na hakijaweza kufikia makubaliano ya muungano huo ama kuelewa masharti yake.

Wiki iliyopita, aliibua shaka kwamba ukosefu huo wa uwazi unaweza kusababisha baadhi ya wagombea kufungiwa nje ya uchaguzi wa Agosti katika dakika za mwisho.

"Wanacheza michezo gani? Mnamo Jumatatu, Mei 9, 2022, chama kitafanya uamuzi kuhusu njia ya kusonga mbele kwa kuzingatia mipango ya kuwatenga wawaniaji wa chama chetu na makataa yaliyowekwa na sheria," Mutua alisema.

Aliongeza;

"Kuna hatari ya wazi na iliyopo kwamba wanaowania katika vyama vya Azimio watanyimwa fursa yao ya kidemokrasia ya kuwa kwenye kura. Hili hatuwezi kulikubali," alisema.

DP Ruto alimkaribisha rasmi gavana huyo kwenye muungano wake.