Vurugu zazuka katika mkutano wa Azimio Mombasa baada ya Sonko kuwasili

Muhtasari
  • Vurugu vyazuka katika mkutano wa Azimio Mombasa baada ya Sonko kuwasili
MIKE SONKO
Image: BRIAN OTIENO

Vurugu vilikumba kwa muda mkutano wa Azimio wa Raila Odinga huko Mkomani mjini Mombasa baada ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuwasili

Magari ya Sonko yaliwasili katika ukumbi wa Mkomani wa mkutano huo mwendo wa saa 3.30 jioni.

Magari yake mawili yalijaribu kuelekea upande wa pili wa ukumbi uliokuwa na watu wengi huku wawaniaji tofauti wakijitambulisha.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho alilazimika kukatiza utambulisho huo mara kadhaa alipokuwa akiwahutubia madereva kutosogeza magari hayo.

"Juma, usisogeze magari, yaweke hapo yalipo, unaenda wapi?" Joho aliendelea kuuliza.

Joho alijaribu kutuliza umati lakini kelele ziliendelea kupanda, huku gari la Sonko likiendelea kupita katikati ya umati.

Mambo yote yalizuka baada ya mawe kuonekana yakiruka kati ya umati, na kuwalazimu polisi kuingilia kati huku wakifyatua risasi hewani kujaribu kutawanya sehemu ya umati iliyokuwa ikizidi kuwa mbaya.

Magari ya Sonko kisha yakageuka huku umati ukitawanyika.