Polisi wamsaka mshukiwa kwa mauaji ya mwanafunzi Kiambu, mwili kutupwa kando ya barabara

Muhtasari
  • Mwili wake ulipatikana umetupwa kando ya barabara karibu na mtaa wa Mburiria mapema Jumamosi asubuhi
Crime Scene

Maafisa wa upelelezi katika Kaunti ya Kiambu wanamsaka mwanamume aliyejulikana kama VDJ Flex ambaye anahusishwa na mauaji ya mwanafunzi wa chuo mwenye umri wa miaka 19.

Purity Wangeci Kiringa anasemekana kuondoka chuoni siku ya Ijumaa ili kumtembelea mpenziwe eneo la Kirigiti, Kaunti ya Kiambu.

Mwili wake ulipatikana umetupwa kando ya barabara karibu na mtaa wa Mburiria mapema Jumamosi asubuhi, ukiwa na majeraha ya kuchomwa kisu na kunyongwa.

Makachero kutoka Idara ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai (DCI) walibaini kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 aliuawa sehemu nyingine na mwili wake kutupwa katika eneo la tukio, ambapo hati zake za utambulisho, matandiko yenye damu na nguo pia zilipatikana.

Kulingana na marafiki zake waliozungumza na wapelelezi, wenzi hao walikuwa na ugomvi hivi majuzi "baada ya kugundua kwamba alikuwa jambazi na kumkabili na ukweli."

Mwili wake ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City jijini Nairobi kusubiri uchunguzi wa maiti yake, huku wapelelezi wakimfuatilia mshukiwa.