Raila akanusha madai ya ODM kupoteza umaarufu Pwani

Muhtasari
  • Alisema chama hicho kimepata matatizo madogo tu kwenye uteuzi wa chama
KInara wa ODM Raila Odinga
Image: George Owiti

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amepuuzilia mbali madai kuwa chama chake kinapoteza umaarufu Pwani.

Akizungumza mjini Mombasa alipokuwa akifungua kituo cha Azimio huko Nyali, Raila alisema ODM ingali shwari Mombasa na eneo kubwa la Pwani.

"Sisi ndio tumeanza. Tunazungumza na watu wetu," alisema.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema wanaoeneza uvumi kwamba ODM inapungua Pwani ni watu wa kuhofia ambao wenyewe wana hofu.

Alisema chama hicho kimepata matatizo madogo tu kwenye uteuzi wa chama.

"Lakini majeraha hayo yanapona taratibu," Raila alisema.

Alisema chama chake kina sera za kufufua uchumi wa Pwani.

Mpeperushaji bendera wa urais wa Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya alisema utawala wake, iwapo atajinyakulia kiti cha urais, utatanguliza utendakazi wa Eneo Maalum la Kiuchumi la Dongo Kundu ili kutoa nafasi za kazi kwa watu wa Mombasa.

Alibainisha wanaoeneza uongo kuhusu ODM ni hao hao wanaodanganya wakaazi wa Mombasa kuwa watarudisha huduma za bandari walikoziiba.