Jacob Ochola: Kutana na mwanaume anayedai kuwa mtoto wa kwanza wa hayati Kibaki

Muhtasari

•Jacob Ochola anasema alikuja kujua kuwa rais huyo wa tatu wa Kenya ndiye babake mzazi akiwa na umri wa miaka 21.

•Ochola anadai kuwa mamake alimtambulisha kwa Kibaki baada ya mwanaume ambaye alidhani ni babake mzazi kuaga dunia.

•Anasema tayari amepiga hatua nyingi katika juhudi za kupata kutambuliwa na familia ya Hayati Kibaki ila hajaweza kufanikiwa.

Image: SCREENGRAB// STANDARD DIGITAL

Mwanaume mmoja mwenye miaka umri wa miaka 61 amejitokeza kudai kuwa yeye ndiye mtoto wa kwanza wa Hayati Emilio Mwai Kibaki.

Jacob Ochola anasema alikuja kujua kuwa rais huyo wa tatu wa Kenya ndiye babake mzazi akiwa na umri wa miaka 21.

Pia anadai kuwa rais huyo wa zamani alimtambua kama mwanawe na aliwahi kukutana naye mara kadhaa tangu mamake alipomtambulisha kwake.

"Mimi ni mtoto wake kuzaliwa. Nimekuwepo kwenye picha. Nimefanya juhudi zote kukutana na baba yangu katika makazi yake ya Muthaiga na ofisi zake zilizoko Nyali. Najulikana sana na walinzi wa GSU wanaolinda pale. Kila wakati nilipotembelea makazi ya babangu sikuenda peke yangu,nilienda na mwanangu na dereva wangu. Pia nilienda Othaya kuona shangazi yangu tukiwa na mwanangu," Ochola aliambia Standard Digital.

Ochola anadai kuwa mamake alimtambulisha kwa Kibaki baada ya mwanaume ambaye alidhani ni babake mzazi kuaga dunia.

"Mama yangu alinifichulia kuwa mwanaume ambaye alifariki sio baba yangu. Aliniambia kuwa huyo ni baba mlezi. Aliniambia kuwa angeenda kuzungumza na babangu kwa kuwa alitaka kuniona kisha anitambulishe. Alifanya hivyo baada ya mwezi. Nilipata fursa ya kukutana na rais wa zamani. Kibaki alikuwa mtu wa kawaida sana kwangu," Alisimulia.

Ochola amesema amekuwa akimtambua Kibaki kama babake tangu Juni mwaka wa 1982 wakati ambapo alitambulishwa kwake. Amesema hatua hiyo ilifanya agundue kuwa yeye sio kutoka jamii ya Luo kama alivyodhani hapo awali.

Pia amedai kuwa alihudhuria misa ya marehemu Lucy Kibaki katika Consolata Shrines na kukutana na rais huyo wa zamani.

"Nilikataa kuenda Othaya kwa kuwa nilikuwa naenda Ethiopia. Baada ya hapo nimepatana na babangu mara kadhaa katika afisi zake Nyali na nimeshiriki mazungumzo naye. Alinihakikishia kuwa ningepata mgao wangu wa mali yake. Nilimwamini baba yangu kwa kuwa nimekuwa nikimwamini," Ochola alisema.

Anasema tayari amepiga hatua nyingi katika juhudi za kupata kutambuliwa na familia ya Hayati Kibaki ila hajaweza kufanikiwa.

Kati ya hatua ambazo Ochola anadai amepiga ni kutembelea dada ya Kibaki na Askofu Mkuu John Njue pamoja na kutafuta huduma za mawakili.

Ochola anadai heshima kubwa ambayo alikuwa nayo kwa hayati ndiyo iliyofanya akose kujitokeza baada yake kufariki.

Hata hivyo amesisitiza kuwa anataka kutambuliwa na kupata mgao wake.