Dereva alikuwa mlevi-Manusura wa ajali ya Kitui wasimulia kilichotokea

Muhtasari
  • "Tulikuwa zaidi ya watu 21 kwenye gari hilo na dereva alikuwa amelewa kwa sababu alipuuza ushauri wetu," alisema mmoja wa walionusurika.
Ajali
Ajali
Image: HISANI

Manusura wa basi  la Kitui wamekatiza kimya chao kuhusiana na kile kilichojiri kabla ya ajali hiyo usiku wa Jumamosi, Juni 4.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumapili, Juni 5, mmoja wa walionusurika alibaini kuwa dereva alikuwa amelewa alipochukua usukani.

Aidha alieleza kuwa gari hilo lilikuwa na mzigo mkubwa kwa vile lilikuwa na watu 21 ingawa limeundwa kubeba abiria 14.

"Tulikuwa zaidi ya watu 21 kwenye gari hilo na dereva alikuwa amelewa kwa sababu alipuuza ushauri wetu," alisema mmoja wa walionusurika.

Mtu mwingine aliyenusurika aliambia runinga ya Citizen kwamba ajali hiyo ilikuwa ya ghafla tangu dereva alipokwepa kukwepa kuligonga gari kabla ya matatu kupinduka na kuacha njia.

Watu tisa waliaga dunia papo hapo huku wengine watatu wakifariki katika hospitali hiyo walipokuwa wakipokea matibabu na kufanya jumla ya waliofariki kufikia 12.

"Alikaribia kugonga gari barabarani lakini alichepuka. Wakati anarudi barabarani, gari lilipinduka na kubingiria. Nilijikuta nje ya gari na watu wametawanyika kila mahali," alithibitisha mwingine.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Kitui Leah Kitheyi alibainisha kuwa ajali hiyo ilitokea saa 11:50 jioni. 

Mmoja wa wanafamilia alibainisha kuwa familia yao bado inakabiliana na mkasa uliowaangamiza jamaa zao waliokuwa wakitoka kwenye sherehe ya ruracio.