Mwanawe Museveni Muhoozi afanya mazungumzo na Rais Uhuru

Muhtasari
  • Muhoozi, ambaye pia ni kamanda wa majeshi ya nchi kavu ya Uganda, alijadili masuala kadhaa ya pande mbili na ya kimataifa yenye maslahi kwa Kenya na Uganda
Muhoozi Kainerugaba na Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni alimtembelea Rais Uhuru Kenyatta Jumatano katika Ikulu ya Nairobi.

Muhoozi, ambaye pia ni kamanda wa majeshi ya nchi kavu ya Uganda, alijadili masuala kadhaa ya pande mbili na ya kimataifa yenye maslahi kwa Kenya na Uganda.

"Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na kurejesha amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," Ikulu iliripoti.

Ziara ya Muhoozi nchini Kenya inajiri huku kukiwa na fununu kwamba anaweza kuwa analenga kumrithi babake Rais Museveni katika uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo.

Mwezi Aprili, Jenerali huyo alizua tafrani nchini Uganda baada ya kufanya tafrija kubwa ya kutimiza miaka 48 ambayo ilihudhuriwa na babake Museveni na Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Baadaye, Muhoozi angedokeza kwamba ana nia ya kugombea Urais.