Msako mkali kuanzishwa barabarani kufuatia ongezeko la ajali

Muhtasari

•Taarifa iliyotolewa Jumatano jioni na Idara ya Huduma ya Polisi inasema kuwa msako huo utang'oa nanga mara moja.

•Mwaka huu pekee Kenya imerekodi vifo 1,968 kufikia sasa. 

Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai.
Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai.
Image: MAKTABA

Idara ya polisi kwa ushirikiano na Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) imeagiza msako mkali kote nchini ili kukomesha magari yanayokiuka sheria na madereva wasiotii Sheria za Trafiki na sheria zingine zinazohusiana.

Taarifa iliyotolewa Jumatano jioni na Idara ya Huduma ya Polisi inasema kuwa msako huo utang'oa nanga mara moja.

"Kwa hivyo, madereva wote wa magari na watumiaji wengine wa barabara wanaombwa kushirikiana na vyombo vya kutekeleza sheria katika ngazi ya kitaifa na kaunti ili kufikia malengo ya mpango huu," Taarifa hiyo iliyotiwa saini na msemaji wa polisi Bruno Shioso inasoma.

Polisi wameagiza magari yote ambayo hayajatimiza matakwa ya Sheria za Trafiki kuondolewa barabarani ili kuepusha usumbufu kwa abiria.

Hatua hii imechukuliwa kufuatia ongezeko la vifo vilivyotokana na ajali za barabarani hapa nchini.

Mwaka huu pekee Kenya imerekodi vifo 1,968 kufikia sasa. Idadi hii inaashiria ongezeko la 9.3% ikilinganishwa na wakati kama huu mwaka uliopita ambapo Kenya ilikuwa imesajili vifo 1,800 kutokana na ajali.

"Inasikitisha kwamba ajali nyingi husababishwa na mambo yanayohusiana na binadamu. Kwa hivyo madereva na watumiaji wengine wa barabara wanakumbushwa kuwa waangalifu na kuwajibika wanaposimamia gari au wakati wowote wanapotumia barabara ya umma kama watembea kwa miguu," Shioso alisema.

Idara ya polisi imesema kuwa ongezeko la ajali ni jambo la kutia hofu ambalo linahitaji kushughulikiwa kwa dharura na washika dau wote.

Wiki hii pekee takriban watu kumi na wawili wameripotiwa kufariki katika ajali zilizotokea Mwingi na Kiambu. Bali na vifo, majeruhi wengi pia wameripotiwa kutokana na ajali nyingi ambazo zimeendelea kushuhudiwa.