Elachi:Kwa nini Uhuru, Ruto lazima warudi nyumbani

Muhtasari
  • Elachi alisisitiza kuwa viongozi wazuri ambao wana nia ya dhati ya Kenya watasaidia kurejesha uthabiti wake wa kisiasa na kiuchumi
Katibu mkuu mwandamizi katika kitengo cha jinsia ya umma, Beatrice Elachi.
Katibu mkuu mwandamizi katika kitengo cha jinsia ya umma, Beatrice Elachi.
Image: Facebook

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amesema kuwa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanahitaji kurejeshwa nyumbani.

Akiongea na NTV siku ya Alhamisi, Elachi alieleza kuwa ili Kenya ipate uvumilivu wa kisiasa ilikuwa imefika wakati maafisa hao wawili wakuu waondoke afisini na kutafuta watu wapya.

Aliongeza kile ambacho Kenya inahitaji ni kuangazia upya na kujenga upya kama ilivyokuwa mwaka wa 2002.

"DP na Rais wangu lazima waende nyumbani na sisemi kwa sababu niko Azimio, nasema hivyo ili tuielekeze tena nchi hii, tuirudishe 2002 na kuanza nayo safari," alisema.

Elachi ambaye anawania kiti cha ubunge cha Dagoretti Kaskazini aliongeza kuwa ni jukumu la kibinafsi kuhakikisha kuwa viongozi makini wanachaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huu.

Elachi alisisitiza kuwa viongozi wazuri ambao wana nia ya dhati ya Kenya watasaidia kurejesha uthabiti wake wa kisiasa na kiuchumi.

Aliteta kuwa kutokana na rasilimali chache zinazopatikana serikali za kaunti na kitaifa lazima zifanye juhudi ili afisi zifanye kazi inavyopaswa.

"Utekelezaji ipasavyo wa sheria utawaongoza wale waliochaguliwa ofisini kwa manufaa ya taifa," aliongeza.