Naivas wapunguza bei ya unga hadi Ksh 99, mafuta ya kula Ksh 669 kwa lita 2

Jumatano rais Uhuru Kenyatta aliwarai wasaga nafaka kukubalu kupunguza bei za unga kutoka 230 hadi 100

Muhtasari

• Duka la jumla la Naivas limekuwa la kwanza kutangaza kupunguzwa kwa bei za bidhaa za unga na mafuta ya kula kweney matawi yake yote nchini.

bei mpya za baadhi ya bidhaa Naivas
bei mpya za baadhi ya bidhaa Naivas

Uongozi wa maduka ya jumla ya vyakula nchini Kenya, Naivas wametangaza kwamba baada ya rais Uhuru Kenyatta kuwarai wasaga nafaka kupunguza bei ya unga ili kujali hali za Wakenya wa chini walala hoi, sasa wao wamepunguza bei ya bidhaa hiyo pamoja na bidhaa nyingine zinazoenda sambamba na unga.

Katika ujumbe walioandika kwenye ukurasa wao wa Facebook, Naivas walitangaza kwamba katika matawi yao kote nchini sasa Wakenya wanaweza kununua mfuko wa kilo mbili wa unga ugali kwa shilingi 99 pekee, wakitaja kupunguza kwa bei hiyo kama maslahi ya kujali taifa.

Naivas walisema kwamba licha ya serikali kupunguza bei ya unga pekee, ila wao kama binadamu wanajua ugali pekee hauliki kwani lazima uambatanishwe na mboga na hivyo pia kwa dhana hiyo wakatangaza kupunguza hadi bei ya mafuta ya kula, na kuwataka wakenya kutembelea maduka yao ili kujinyakulia ofa hizo kabambe.

“Mnajua serikali imefanya ile kitu kwa bei ya unga but tunajua lazima upike mboga pia kwa hivyo tumecheza kama sisi kwa upande wa mafuta. Ni unga utatajia, mafuta ya kula au zote? #Taifa,” Naivas Waliandika kwenye Facebook yao.

Hizi bila shaka zinakuja kama taarifa njema kwa wapenzi wa ugali baada ya serikali kutangaza siku mbili zilizopita kwamba bei ya unga pakiti ya kilo 2 itapungua kutoka bei ya sasa ya shilingi 230 hadi shilingi 100.

Wasaga nafaka walikaidi agizo hilo na kumlazimu rais Uhuru Kenyatta kuhutubia umma jumatano alasiri na kuwarai wasaga nafaka kupunguza bei hiyo kwa kujali maslahi ya Mkenya wa maisha ya kadri kwani ruzuki katika mahindi ya kuagizwa kutoka nje ilikuwa inatarajiwa kutoka kwa mfuko wa serikali kuu.