Kenya yatoa siku saba kwa Facebook kujielezea kuhusu udhibiti dhaifu wa maudhui

NCIC imetishia kusimamisha matumizi ya Facebook kwa madai ya kukiuka sera za matamshi ya chuki.

Muhtasari

•Tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa nchini imetishia kusimamisha matumizi ya mtandao wa Facebook kwa madai ya kukiuka sera za matamshi ya chuki.

•Global Witness na Foxglove, inasema kwamba Facebook ilishindwa kugundua matangazo yenye maudhui ya uchochezi yaliyochapishwa kwa Kiingereza na Kiswahili.

Image: BBC

Tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa nchini Kenya imetishia kusimamisha matumizi ya mtandao wa Facebook kwa madai ya kukiuka sera za matamshi ya chuki.

Tume hiyo ya Kitaifa inasema imeiandikia Meta ikitaka majibu kwa madai ya udhibiti dhaifu wa maudhui kwenye Facebook kabla ya uchaguzi wa mwezi ujao.

Kamishna wa Ttume Dkt. David Makori alikuwa akijibu matokeo ya ripoti ya Global Witness na Fox Glove ambayo ilionyesha kuwa Facebook imeshindwa kudhibiti maudhui kwenye jukwaa lake kutokana na udhibiti dhaifu.

"Ikiwa Facebook haitatii mahitaji ambayo tumeweka ndani ya siku saba, tutapendekeza wasitishe shughuli zao. Hatutaruhusu Facebook kuhatarisha usalama wetu wa taifa”, Makori alisema.

Tume haina mamlaka ya kusimamisha Facebook lakini inaweza tu kupendekeza kwa mamlaka ikiwa kampuni itashindwa kufuata miongozo kama ilivyoainishwa katika sheria.

Ripoti ya mashirika ya utetezi ya Global Witness na Foxglove, inasema kwamba kampuni hiyo kubwa ya mitandao ya kijamii ilishindwa kugundua matangazo yenye maudhui ya uchochezi kwenye jukwaa lake yaliyochapishwa kwa Kiingereza na Kiswahili.

Wakati wa uchunguzi, watafiti waliwasilisha matangazo 20 yenye lugha ya chuki kutoka katika uchaguzi wa 2007 yaiyochapishwa katika lugha zote mbili. Ripoti hiyo inasema matangazo yote yaliyowasilishwa yaliidhinishwa isipokuwa moja la Kiingereza kwa kutofuata miongozo yake kuhusu matamshi ya chuki.

Global witness inasema matangazo hayajawahi kuchapishwa kwenye Facebook lakini walishangazwa na namna yalivyopita bila kutambuliwa.

Facebook haijajibu matokeo ya ripoti hii.

Mnamo Julai, kampuni ya teknolojia iliripoti kuwaondoa watumiaji 37,000 kwa kuchochea matamshi ya chuki na 42,000 kwa kukiuka ghasia na sera zake za uchochezi wakati wa uchaguzi wa Agosti.

Kampuni hiyo pia ilisema kuwa imekataa matangazo 36,000 ya kisiasa kwa kutofuata sheria zake za uwazi.