Tume ya huduma kwa police NPS imetoa wito kwa Wakenya wote kurudi kazini na kujenga uchumi wa taifa baada ya wiki iliyojawa na matukio mbali mbali ya uchaguzi mkuu.
Kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, NPS iliwaomba Wakenya kukubali na matokeo na kusonga mbele pamoja kama wakenya watu wamoja wapenda amani.
“Turudi kazi, tujenge nchi. Upigaji kura uko nyuma yetu na tunafurahi kwamba zoezi la kitaifa halikufanyika bila matukio mabaya katika sehemu nyingi za nchi. Ni wakati sasa wa kuanza shughuli nyingine za uzalishaji mali katika kujenga taifa huku kujumlisha kura kukiendelea,” NPS iliwarai Wakenya.
Tume hiyo iliwashukuru Wakenya kwa ushirikiano mzuri wa kudumisha amani kipindi cha uchaguzi mkuu na kuwarai kuzidi na amani hiyo huku tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC ikiendelea kupokea matokeo ya chaguzi katika sehemu mbali mbali za nchi na ujumulishaji ukiendelea katika kituo kikuu cha kitaifa kilichopo Bomas, Nairobi.
“Tunaupongeza umma kwa kuunga mkono juhudi zetu za kufanikisha uchaguzi wa amani, huru na wa haki. Tunafuraha kwamba Wakenya wengi wamerejea kwenye mihangaiko yao tofauti huku wakingoja tamko la tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC,” NPS ilizidi kusema.
Awali tume hiyo iliwahakikishia amani Wakenya wote haijalishi sehemu walipo huku matokeo ya chaguzi hizo yakiendelea kupeperushwa moja kwa moja katika runinga mbali mbali humu nchini. NPS ilisema kwamba inaendelea kufanya kazi usiku na mchana bila kupepesa jicho kuhakikisha matokeo hayo yanatolewa kwa wakati.
“Usalama umeimarishwa katika eneo zima ili kuhakikisha kuwa matokeo na nyenzo zote za uchaguzi zinawasilishwa ipasavyo. Jeshi la Polisi nchini linathamini juhudi za kila chombo na hasa linawataka wananchi kuendelea kusalimisha taarifa kwa vyombo vya usalama, na pia kuendelea kudumisha utulivu,” NPS ilitoa wito.