Kalonzo ajiondoa kutoka kinyang’anyiro cha spika wa seneti muda mchache kabla ya uchaguzi

Bado haijabainika sababu kuu ya Kalonzo kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha spika wa seneti.

Muhtasari

• Hatua hiyo ya Kalonzo ilitangazwa na katibu wa Seneti Jeremiah Nyegenye.

Muungano wa Azimio umepata pigo baada ya mgombea wa muungano huo kwa wadhifa wa spika wa seneti Kalonzo Musyoka kujiondoa kutoka kinyang’anyiro hicho.

Hatua hiyo ya Kalonzo ambaye pia ni kinara wa chama cha Wiper ilitangazwa na katibu wa Seneti Jeremiah Nyegenye.

Nyegenye alisema kwamba ofisi yake ilikuwa imepokea barua asubuhi siku ya Alhamisi kutoka kwa Kalonzo akiondoa azma yake.

Maseneta katika muungano wa Azimio siku ya Jumatano walikuwa wameafikia kwa kauli moja kumuunga mkono Kalonzo kwa wadhifa wa Spika wa seneti.

Aliyekuwa gavana wa Kilifi Amason Kingi ambaye anapendekezwa na muungano wa Kenya Kwanza alikuwa mpinzani mkuu wa Kalonzo.

Mapema Jumahili Kalonzo alikuwa amechukuwa stabadhi za kuania wadhifa wa spika katika bunge la kitaifa na Seneti lakini akabadili mawazo na kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha spika wa bunge la Kitaifa ili awanie nafasi ya spika wa seneti.

Bado haijabainika sababu kuu ya Kalonzo kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha spika wa seneti.