Moses Kuria kufunga akaunti ya Facebook baada ya Ruto kuapishwa

Hii akaunti kazi yake imekwisha - Moses Kuria.

Muhtasari

• Akaunti hii itafutwa kabisa Jumatano tarehe 14 Septemba 2022 saa 18:00 - Kuria

• Akiifunga, atakuwa amejiunga na Winnie Odinga na Fred Matiang'i ambao walifunga zao za Twitter jana.

Moses Kuria atangaza kufunga akaunti yake ya Facebook
Moses Kuria atangaza kufunga akaunti yake ya Facebook
Image: Facebook

Aliyekuwa mbunge wa Gatundu South Moses Kuria amesema kwamba kuanzia Jumatano ya Septemba 14 jioni, ataifuta kabisa akaunti yake ya Facebook.

Kuria ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Kazi na ambaye alikuwa mgombea wa ugavana Kiambu ila akapoteza kwa aliyekuwa seneta Kimani Wamatangi alisema kwamab hatua yake ya kuifuta akaunti yake ni kwa sababu lengo lake limetimia.

Licha ya kuwa mbunge wa Uhuru Kenyatta, Kuria alikuwa na misimamo mikali dhidi ya rais huyo mstaafu na alikuwa mstari wa mbele kumtetea na kumpigia debe rais wa sasa William Ruto.

Kuria alisema akaunti hiyo itakunywa maji jioni ya leo baada ya kumaliza dhamira yake ambayo ilikuwa ni kumpigia debe William Ruto na maadamu ashashinda na kuapishwa kama rais wa tano, basi akaunti hiyo nayo imemaliza kazi yake kuu.

“Lengo langu limetimia. Rafiki yangu mkubwa William Ruto ni Rais wa 5 wa Jamhuri ya Kenya. Akaunti hii itafutwa kabisa Jumatano tarehe 14 Septemba 2022 saa 18:00. Ilikuwa kushirikiana mzuri jamani. Adios!” Kuria aliandika kweney akaunti hiyo.

Moses Kuria kufunga akaunti yake
Moses Kuria kufunga akaunti yake

Kuria sasa atajiunga na baadhi ya watu mashuhuri ambao walifunga akaunti zao akiwemo mtoto wa kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, Winnie Odinga aliyeifunga akaunti yake ya Twitter jana, aliyekuwa Waziri wa masuala ya ndani Dkt Fred Matiang’i ambaye pia akaunti yake ya Twitter ilifungwa jana na rais mstaafu Uhuru Kenyatta aliyesema alifunga akaunti yake ya Twitter miaka miwili iliyopita.