Raila arejea nchini kimya kimya, asuta mahakama kwa kutupilia mbali kesi yake

Tunataka kusubiri na kuona maelezo haya yatahusu nini - Raila alisema.

Muhtasari

• Raila aliyejawa na hasira alisema kuwa yeye wala Wakenya hawatatishwa na mahakama ya upeo dhidi ya kuzungumzia uamuzi wake potofu.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Hisani

Mjumbe wa Umoja wa Afrika Raila Odinga amewasili nchini kimya kimya baada ya kuwa nje kwa siku chache. Kiongozi huyo wa ODM aliwasili nchini siku ya Alhamisi na kuelekea Mombasa moja kwa moja kwa chakula cha mchana cha Gavana Abdulswamad Nassir huko Sarova Whitesands.

Hata hivyo, hakuhudhuria hafla ya kuapishwa ambayo ilipambwa na viongozi wengine wa Azimio akiwemo aliyekuwa Gavana Hassan Joho, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kinara wa Narc Kenya Martha Karua miongoni mwa wengine.

Hii ni mara yake ya kwanza kuonekana hadharani baada ya William Ruto kuapishwa kuwa rais wa tano wa Kenya. Katika taarifa ya awali, Raila alisema alialikwa kwenye hafla hiyo lakini kwa bahati mbaya atakuwa hayupo.

Katika hotuba yake ya kwanza tangu mahakama ya upeo kutupilia mbali ombo lake la kutaka ushindi wa Ruto kubatlishwa, Odinga alisema haoni haja kwa nini Wakenya waamke 2027 kupiga kura ikiwa walichokiona kwenye uchaguzi wa Agosti kitarudiwa.

Raila alisema yeye na Wakenya wengine wengi wanasubiri kwa hamu kusikia ni hoja gani ya kina ambayo Mahakama ya Juu itatoa kuhusu uamuzi wake kuhusu ombi lake la urais ambalo walitupilia mbali kama halina msingi.

"Tunataka kusubiri na kuona maelezo haya yatahusu nini," Raila alisema.

"Kwa nini wanawake, wazee (na) walemavu wapange foleni kwa saa nyingi ili kupiga kura zao wakati mwisho wa siku ni mamluki kutoka Venezuela anayeitwa Bw Jose Camargo ambaye hatimaye ndiye atakayeamua nani awe rais wa nchi hii?" Raila aliuliza.

Kiongozi huyo wa ODM alisema inashangaza kwamba mahakama ilionyeshwa ushahidi wa jinsi mgeni huyo alivyoingilia kura kwenye tovuti ya umma lakini mahakama ikapuuzilia mbali jambo hilo kama hewa moto.

"Inawezekanaje kuwa kifaa kinasambaza matokeo kutoka Mlima Elgon na dakika nane baadaye kusambaza matokeo kutoka Nyeri? Je, hilo si jambo la kushangaza?” Raila aliuliza.

Raila aliyejawa na hasira alisema kuwa yeye wala Wakenya hawatatishwa na mahakama ya upeo dhidi ya kuzungumzia uamuzi wake potofu.

Alikariri kuwa anaheshimu uamuzi wa mahakama lakini hakubaliani nao. Mahakama ya majaji saba ilisema itatoa uamuzi wake kamili kuhusu ombi la Raila ndani ya siku 21.