Jinsi hayati Mwai Kibaki alivyogawa utajiri wake yafichuliwa

Maelezo ya jinsi aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya alivyogawa mali yake yameibuka.

Muhtasari

•Imebainika kuwa marehemu Kibaki aligawa utajiri wake miongoni mwa watoto wake wote  kwa usawa.

•Hata hivyo aliwafungia wenzi wa wanawe dhidi ya kurithi sehemu yoyote ya mali yake.

Aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya hayatii Mwai Kibaki
Image: MAKTABA

Aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya hayati Mwai Kibaki bila shaka alikuwa tajiri huku akiwa amehudumu uongozini kwa takriban miongo sita.

Ingawa thamani ya utajiri wake bado ni kitendawili hadi leo, maelezo ya jinsi alivyogawa mali yake yameibuka.

Katika wosia alioandika mwaka wa 2016, miaka mitatu tu baada ya kukabidhi vyombo vya mamlaka kwa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, imebainika kuwa marehemu Kibaki aligawa utajiri wake miongoni mwa watoto wake kwa usawa.

Katika wosia huo, aliwateua watoto wake Judy Wanjiku, Jimmy Kibaki, David Kagai na Anthony Githinji kuwa waridhi wa mali yake.

Ombi maalum la Kibaki katika wosia wake lilikuwa mgawanyo sawa wa mashamba na pesa taslimu kwenye akaunti zake zote za benki.

Rais huyo wa zamani zaidi vitu vyake vya kibinafsi zote zikiwemo karatasi kukabidhiwa Mwai Kibaki Foundation.

Kulingana na wosia wa Kibaki, aliamuru watoto wake wapokee marupurupu kutoka kwa mali fulani.

Hata hivyo aliwafungia wenzi wa wanawe dhidi ya kurithi sehemu yoyote ya mali yake.

"Kufuatia kifo changu mwenyewe basi watoto wao wa moja kwa moja wa damu (lakini si wenzi wao wa maisha) watapokea faida ya mzazi wao, ikiwa zaidi ya mmoja katika hisa sawa," ulinukuu wosia huo.

Hata hivyo, thamani ya rais huyo wa zamani haijafichuliwa.

Lakini hata maelezo ya uridhi yanapojitokeza, watu wawili wamejitokeza kudai kuwa ni watoto wa Kibaki.

Katika karatasi za mahakama, JNL inadai kuwa binti mkubwa wa Kibaki.

JNL anadai kwamba alizaliwa wakati mamake na Kibaki walikuwa wanafunzi huko London.

Katika ombi lake mbele ya mahakama ya familia, alidai kuwa ridhaa yake haikuombwa kabla ya hati za urithi kuwasilishwa kortini.

Jacob Ocholla ambaye pia anadai kuwa mtoto wa Kibaki pia anataka kujumuishwa katika sehemu ya mali yake.

Hii inafuatia notisi ya gazeti la serikali ambayo ilichapishwa kwa yeyote anayepinga wosia huo.

Kibaki aliwahi kuwa rais wa tatu wa Jamhuri ya Kenya kutoka mwaka wa 2002 hadi 2013.

Alifariki Aprili 2022 na kuzikwa nyumbani kwake Othaya, kaunti ya Nyeri. Kibaki aliacha nyuma watoto wanne.