logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Chama cha ODM chamteua mshona viatu kuwakilisha walemavu Siaya

Kazi yake imekuwa ikimwingizia  kati ya Shilingi 150 ama 200 kwa siku.

image
na

Habari20 September 2022 - 07:31

Muhtasari


•Uteuzi wa Fredrick Odhiambo Oloo uliwapiga butwaa wakaazi walioamini nafasi za uteuzi za chama zimetengwa kwa ajili ya familia na jamaa wa wanasiasa wakubwa ama wale wanaojuana.

•Habari za uteuzi wake zilipotangazwa, fundi huyo alikuwa katika duka lake la Bondo Kolalo akitengeneza patipati zilizokuwa zimekatika.

Chama cha ODM kimemteua mshona viatu mwenye umri wa miaka 47 kutoka kijiji cha Masiro, eneo la Ugenya Mashariki kuwakilisha vilema katika bunge la kaunti la siaya.

Uteuzi wa Fredrick Odhiambo Oloo uliwapiga butwaa wakaazi walioamini nafasi za uteuzi za chama zimetengwa kwa ajili ya familia na jamaa wa wanasiasa wakubwa ama wale wanaojuana 

Odhiambo ni mmoja wa viongozi waliojitokeza kwenye mkutano wa awali ulioandaliwa nje ya bunge la kaunti Jumatatu kabla ya hafla ya uapishaji itakayofanyika leo Jumanne.

Akiwa amevaa shati la samawati lililoraruka kola, miguu tupu na nywele iliyonyolewa vizuri, kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake Odhiambo aliingia kwenye uwanja wa bunge la kaunti akitumia magongo  yaliyomsaidia kutembea.

Kinyasa cha kijani kibichi kilichokuwa na mifuko ya pembeni ya rangi ya machungwa kilifunika kiuno chake.

Habari za uteuzi wake zilipotangazwa, fundi huyo alikuwa katika duka lake la Bondo Kolalo akitengeneza patipati zilizokuwa zimekatika.

Kazi hiyo inamwingizia  kati ya Shilingi 150 ama 200 kwa siku.

“ Bado niko katika hali ya mshtuko, fundi wa viatu, kilema kama mimi, sasa anatambulika kama ‘Mheshimiwa’.nakipa Chama cha ODM shukrani zisizo na mwisho,”alisema.

Bidii ya kuwakilisha maslahi ya vilema ilikua dhahiri kwenye sauti yake.

“Najua shida zinazowakumba watu kama mimi kwenye jamii. Nikishaapishwa, nitarudi kijijini ili nikawaongoze kujadili suluhisho za shida zao,”alisema.

Odhiambo alisema uteuzi wake ulitokana na uaminifu  na upendo wake kwa Gavana James Orengo na Chama cha ODM.

Alisema, yeye kama fundi wa viatu alipenda kuzungumza siasa katika  kazi yake na aliwaomba watu kuwapa mkono Orengo na Raila Odinga.

Alisema Orengo alimzawadi mikongojo aliyokuwa akitumia na aliahidi kumteua.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved