Miili mitatu zaidi yatolewa kutoka Mto Yala

Miili hiyo mitatu imetolewa kutoka Mto Yala karibu na eneo moja ambapo miili zaidi ya 30 ilitolewa.

Muhtasari

•Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Africa Hussein Khalid alisema wakaazi wanaendelea kutoa miili zaidi kutoka kwenye  mto huo.

•Polisi mnamo Januari walianzisha uchunguzi kubaini kitendawili kuhusu miili iliyotupwa katika Mto Yala katika kaunti ya Siaya.

Maafisa wa polisi walipata mwili kutoka Mto Yala mnamo Machi 27, 2022.
Maafisa wa polisi walipata mwili kutoka Mto Yala mnamo Machi 27, 2022.
Image: AKELLO ODENYO

Miili mitatu ya watu wasiojulikana imetolewa kutoka mto Yala mwezi Septemba.

Akizungumza na wanahabari  Ijumaa, Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Africa Hussein Khalid alisema wakaazi wanaendelea kutoa miili zaidi kutoka kwenye  mto huo.

"Hivi majuzi kama mwezi huu, miili bado inatolewa kutoka mtoni. Mili mitatu mwezi huu ambayo bado tunajaribu kuitambua,” Khalid alisema.

Miili hiyo mitatu imetolewa kutoka Mto Yala karibu na eneo moja ambapo miili zaidi ya 30 ilipatikana ikiwa imetupwa karibu na Maporomoko ya Ndanu, mwanzoni mwa mwaka huu.

Miili hiyo ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Kaunti Ndogo ya Yala ikisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti.

“Tunaitaka serikali hii mpya kushughulikia suala la kutoweka kwa watu na mauaji ya kiholela haraka iwezekanavyo. Tabia mbaya imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu sana," Khalid alisema.

Polisi mnamo Januari walianzisha uchunguzi kubaini kitendawili kuhusu miili iliyotupwa katika Mto Yala katika kaunti ya Siaya.

Watu wanaoishi kando ya kingo za mto Yala walikuwa wametoa wasiwasi juu ya kuongezeka kwa idadi ya maiti ambazo hazijatambuliwa zilizochukuliwa kutoka kwa mto huo.

Wakazi wanashuku kuwa magari mawili—double cabin nyeusi na Toyota Probox nyeupe—yaliweza kutumika kusafirisha miili hiyo kutupwa mtoni.

 "Magari hayo mawili yameonekana mara kadhaa karibu na Maporomoko ya Ndanu, na tunaamini ni magari ambayo waliohusika na vifo wamekuwa wakitumia kusafirisha miili na kuitupa mtoni," alisema Okite Okero, mchukuaji wa maiti kutoka mto Yala.

Wanaharakati wa haki za binadamu katika harakati ya kutafuta ukweli walidai kuwa walifanya ugunduzi wa kushtua wa miili inayoelea kwenye magunia huku baadhi ya waliouawa wakiwa wamefunikwa vichwa na mifuko ya nailoni.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso alitembelea eneo la tukio mnamo Januari kabla ya timu kutoka DCI kutumwa kufanya uchunguzi wa kitaalamu na kusaidia katika utambuzi wa miili na sababu ya kifo.

Polisi walithibitisha kuwa tangu Januari mwaka jana, miili 20 ilikuwa imetolewa kutoka Mto Yala.

"Tunashuku kuwa waathiriwa wameuawa kwingine na miili kutupwa hapa," OCPD wa Yala Charles Chacha alisema kwa simu.

"Miili hiyo inajaza chumba cha kuhifadhia maiti chenye uwezo wa kubeba miili 17 katika hospitali ya kaunti ndogo ya Yala na inafaa kutupwa," alisema.