Waziri Magoha ataka mitandao ya video chafu kufungwa ili kuwalinda watoto

Waziri huyo alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa tamasha la muziki Kisumu.

Muhtasari

• Msomi huyo mwenye misimamo mikali pia alisema hajali kuitwa mpinzani  kwa kupinga mitandao hii yenye utovu wa maadili.

Waziri wac elimu profesa George Magoha
Waziri wac elimu profesa George Magoha
Image: THE STAR//MAKTABA

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha ameitaka serikali kupiga marufuku mitandao yote ya kijamii ambayo inaonesha video chafu kama njia moja ya kuwalinda watoto kutokana na utoro huo.

Akizungumza kwenye hafla ya kufungua tamasha la muziki kaunti ya Kisumu Jumatatu, waziri huyo alitoawito kwa mamlaka husika kutafuta njia mbadala ya kudhibiti mitandao hiyo inayowapa watoto mafunzo potovu.

‘Hata kama tunajivunia uhuru wa kila kitu ikiwemo mitandao ya kijamii, mitandao yenye picha chafu ni sharti izimwe haraka iwezekanavyo,’’ Magoha alisema.

Msomi huyo mwenye misimamo mikali pia alisema hajali kuitwa mpinzani  kwa kupinga mitandao hii yenye utovu wa maadili.

‘’Wakati nilisema haya, walisema hapana, mimi ni mpinzani lakini nataka kuwa mpinzani kwa fikira za watu’’ waziri Magoha aliongeza.

Hata hivyo Magoha aliwaomba Wakenya kumuunge mkono kwa pendekezo lake la kufunga mitandao hiyo ambayo kwa maoni yake inahatarisha usalama wa watoto mitandaoni.

Aliendelea kudokeza kwamba hii si mara ya kwanza kutoawito huo kwani mnamo Juni 2020 alihimiza mitandao hiyo kufungwa ila akapuuziliwa mbali lakini sasa matokeo yake yamekuja kuwa ni ongezeko la mimba za mapema kwa watoto wa shule.

 ‘Usituambie kwa sababu ipo Marekani nasi tunafaa tuwe nayo. Kunazo nchi za Afrika na Asia ambazo zimefunga mitandao hii na mila zao ni za kuvutia,’’ Waziri Magohaalionesha kuchukizwakwake.

Waziri huyu anaomba serikali ya rais Ruto kupa kipaumbele suala la usalama wa watoto dhidi ya mitandao kama hii inayonuia kuwapotosha kitabia na kimaadili pia.

Magoha aliteuliwa kama waziri wa elimu na rais mstaafu Uhuru Kenyatta mwaka 2017 baada ya waziri Dkt. Fred Matiang’i kuhamishwa kutoka wizara hiyo kuelekea katika wizara ya usalama wa ndani.

Magoha ambaye amekuwa mtetezi mkubwa wa mtaala mpya wa CBC mpaka sasa anashikilia wizara hiyo huku taifa likisubiri rais mpya William Ruto kuteua baraza lake jipya la mawaziri.