Aliyekuwa mbunge wa Cherangany Kipruto Arap Kirwa amesema Raila Odinga anaweza kuania urais mwaka wa 2027 na huenda akawa maarufu hata zaidi.
Kulingana na Kirwa, Odinga licha ya umri wake bado kuna matumaini yake kuwa rais wa sita wa jamhuri ya kenya Katika uchaguzi ujao.
''Raila atakuwa na umri wa miaka 82 hivi, na hii ina maana kwamba anaweza na ushawishi na ili kuchaguliwa huhitaji kuwa na nguvu nyingi, unahitaji tu kuwepo na kuiana na matakwa ya wananchi,'' Kirwa alisema Jumatano.
Raila ambaye alikuwa akiwania urais kwenye uchanguzi wa Agosti 9 mwaka huu,hajatangaza hatua yake inayofuata katika ulingo wa siasa.
Iwapo Raila atawania urais, 2027 basi itakuwa mara yake ya sita baada ya kujaribu kwa mara tano.
Akiwa mbunge na kiongozi shupavu wa upinzani mwaka 1997, aligombea urais na kushindwa na Rais mstaafu marehemu Daniel Moi aliyezoa kura milioni 2.45, akifuatiwa na marehemu Rais mstaafu Mwai Kibaki wa Democratic Party, ambaye alikuwa na kura milioni 1.9.
Mnamo 2002, Raila aliweka kando azma yake ya urais na badala yake akamuunga mkono Kibaki, ambaye alishinda.
Mwaka 2007, alijiunga na kinyanganyiro cha urais tena akikabiliana na Kibaki ambaye alitangazwa mshindi kwa kura milioni 4.58 dhidi ya milioni 4.35 zake.
Uchaguzi huo ulifuatiwa na ghasia za baada ya uchaguzi zilizogharimu maisha ya zaidi ya watu 1,000 nakusababisha zaidi ya 500,000 kuyahama makazi yao baada ya Raila kukataa matokeo.
Mwaka 2013, Raila alikuwa kwenye kinyanganyiro cha urais lakini safari hii akipambana na Uhuru Kenyatta, mtoto wa mpinzani wa babake wa kisiasa baada ya uhuru mwaka 1963. Kwa wakati wa pili katika kiti cha urais, Uhuru alishinda uchaguzi kwa kura milioni 6.17, dhidi ya milioni 5.34 za Raila.
Mwaka 2017, Uhuru alitafuta muhula wa pili ambapo alikabiliana na Raila ambaye alipoteza tena.
Uchaguzi huo hata hivyo ulibatilishwa na Mahakama ya Juu lakini Raila akasusia marudio. Katika kura za mwezi uliopita, Raila aliamua kugombea kwa mara ya tano akikabiliana na William Ruto ambaye alikuwa naibu rais Uhuru kwa miaka 10.
Agosti 15, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Naibu Rais William Ruto Rais mteule baada ya kuwashinda Raila na wagombea wengine wawili katika kura ya urais ya Agosti 9.
Ruto alitangazwa mshindi kwa kura milioni 7.1 sawa na asilimia 50.49 ya kura zilizopigwa, dhidi ya kura 6.9 za Raila, sawa na asilimia 48.85 ya kura zilizopigwa.
Hata hivyo, Raila alikataa matokeo hayo na kuyataja kama batili na kwenda katika Mahakama ya Juu.
Mahakama ya Juu iliidhinisha ushindi wa Ruto na akaapishwa wiki jana kama rais wa tano wa Kenya.
Kufikia sasa Raila bado hajatangaza kuhusu mkondo wake kisiasa .