Uganda yashtaki ODM katika mahakama ya EACJ dhidi ya kuita Museveni dikteta

Mfanyibiashara Paul Bamutaze alielekea katika mahakama hiyo kutaka haki dhidi ya matamshi ya Junet Mohammed na John Mbadi kusema Museveni ni katili.

Muhtasari

• Tutamlinda Rais wetu, Kaguta Museveni, NRM Online, William Ruto, na jumuiya, dhidi ya mashambulizi ya aina hii - Bamutaze.

Mahakama ya haki ya EACJ
Mahakama ya haki ya EACJ
Image: Paul Bamutaze//Twitter

Mfanyibiashara mashuhuri nchini Uganda, Paul Bamutaze aligonga vichwa vya habari nchini Kenya baada ya kudai kwamba anaelekea mahakamani kuwashtaki baadhi ya viongozi wa chama cha ODM kwa kumuita rais Museveni mtu katili.

Mfanyibiashara huyo amabye ni mwandani wa karibu wa rais Museveni alielekea katika mahakama ya haki ya ukanda wa Afrika Mashariki EACJ kuwashtaki viongozi hao kwa kile alisema ni kumchafulia jina rais wao kwa kumbatiza majina ambayo hayaendani na vitendo vya uongozi wake.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Bamutaze alidokeza leo kwamba kesi hiyo sasa imeng’oa nanga rasmi katika mahakama hiyo iliyopo Arusha Tanzania.

“Kesi dhidi ya wabunge wa ODM dhidi ya rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, na mwanawe Muhozi Kainerugaba imeanza leo katika mahakama ya haki ya EACJ jijini Arusha. Ningependa kusisitiza kwamba rais Museveni ni kiongozi aliyechaguliwa na si dikteta kama ilivyoelezwa na Junet Mohammed na wenzake,” Bamutaze aliandika kwenye Twitter.

Mfanyibiashara huyo alipakia klipu ikiwaonyesha baadhi ya viongozi wa ODM walimzomea rais Museveni na kusema kwamba ni sharti wamtetee rais wao kwa njia yoyote ile dhidi ya matamshi kama hayo.

“Tutamlinda Rais wetu, Kaguta Museveni, NRM Online, William Ruto, na jumuiya, dhidi ya mashambulizi ya aina hii ambayo yanaharibu maendeleo kuelekea Shirikisho la Kisiasa la EAC! EACJ inapoanza kusikilizwa kwa Kesi yangu dhidi ya chama cha ODM, tunaomba haki itendeke,” Bamutaze aliandika jana jioni.