Una hadi November 2022 kubadilisha pasipoti yako ya zamani

Kenya kuhamia EAC kwa pasipoti mpya ya kielektroniki ifikapo Novemba 30

Muhtasari

• Kenya imekuwa ikitoa pasipoti za kizazi cha zamani kama sehemu ya kujitolea kwa kuhamia kwenye pasipoti mpya ya EAC

Wakenya wana hadi mwezi Novemba mwaka huu kutafuta paspoti za kisasa za  kielektroniki.

Hii ni kutokana na taarifa ya mkurugenzi Mkuu wa  idara ya Uhamiaji Alexander Muteshi siku ya Alhamisi, akiwataka wakenya kupata pasipoti za kisasa kufikia Novemba 30, 2022.

Hii ilikuwa mara ya nne kutangazwa kwa tarehe ya mwisho ya matumizi ya paspoti za zamani, muda wa mwisho wa matumizi ya paspoti hizo ulikuwa umewekwa mwezi Machi mwaka 2019 lakini muda huo ukaongezwa na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta.

Tarehe ya mwisho ya kuondolewa kwa paspoti za zamani kwa mataifa ya Afrika Mashariki ni Novemba 2022, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri wa jumuia hiyo uliofanyika mjini Arusha, Tanzania mwaka jana.

''Idara ya Huduma za Uhamiaji ingependa kufahamisha umma kwa ujumla kwamba Kenya italazimika kuhamia kikamilifu kwenye paspoti mpya ya kielektroniki za kibayometriki  ifikiapo tarehe 30 Novemba 2022," Muteshi alisema.

"Kwa hivyo Wakenya wanashauriwa kupata pasipoti mpya za kielektroniki ili kuepuka usumbufu wowote."

Hii inamaanisha kuwa pasi za bluu-kijani zitakuwa batili.Serikali ilikuwa imeongeza makataa ya hapo awali kutoka Desemba 31 mwaka jana hadi Novemba 2022, ili kuruhusu Wakenya zaidi kupata pasipoti mpya za kielektroniki.