Mifupa mikavu na nguo zinazoaminika kuwa za wataalam wa IT wa India na dereva wao zapatikana

Raia hao wa India walipotea katika mazingira tatanishi Julai mwaka huu ,ambapo sasa kupotea kwao kunahusishwa na kikosi cha SSU kilichovunjiliwa mbali na rais.

Muhtasari

• Baada ya kupatikana katika msitu wa Aberdare, vilisafirishwa hadi Nairobi katika maabara kuu ya DCI kwa uchunguzi zaidi.

Mifupa inayokisiwa kuwa ya wataalamu wa IT kutoka India na dereva wao yapatikana
Mifupa inayokisiwa kuwa ya wataalamu wa IT kutoka India na dereva wao yapatikana
Image: Maktaba

Wiki hii imekuwa na minong’ono mikali haswa baada ya rais William Ruto kutoa amri ya kuvunjiliwa mbali kwa kikosi maalumu cha upelelezi SSU ambacho kilihusishwa na maujai na kutoweka kwa raia wawili wa India ambao walitoweka mapema mwaka huu kwa njia za utata.

Baada ya kuvunjiliwa mbali kwa kikosi hicho, maafisa wake waliamrishwa kuripoti katika afisi za DCI na mchakato wa kuanza kuhojiwa kwao uling’oa nanga katika kile kinaaminika kuwa ni kutaka kujua kilichotokea kwa raia hao wawili wa India pamoja na dereva wao Mkenya ambao tangu kutoweka kwao hadi leo hawajawahi julikana waliko au hata miili yao kupatikana kama kweli waliuawa.

Msako mkali ulianzishwa ambapo vyombo vya habari vya humu nchini sasa vinaripoti kwamba mifupa mikavu, mikanda pamoja na nguo, vyote vinavyoaminika kuwa vya watatu hao vimepatikana katika msitu wa Aberdare kaunti ya Nyeri na kusafirishwa kuja Nairobi katika maabara kuu ya serikali kwa ajili ya vipimo zaidi ili kutathmini kama kweli ni wao.

Msako huo ulianzishwa siku tatu zilizopota ambapo zaidi ya maafisa 100 wa polisi walitumwa katika msitu wa Aberdare kuwatafuta Mohamed Zaid Sami Kidwai, Zulfiqar Ahmad Khan na dereva wao, Nicodemus Mwania Mwange waliotoweka kwa njia za utatanishi Julai 25.

Maafisa hao walichukua ushahidi kwa usalama kabla ya sampuli ya DNA iliyopangwa ili kubaini ikiwa ni wa watatu hao. Maafisa wa SSU wanaohusishwa na kutoweka na kifo cha watatu hao wanatarajiwa kufika mbele ya maafisa wa upelelezi wa Kitengo cha Masuala ya Ndani wanaoshughulikia kesi hiyo.

Maafisa kumi walikuwa wamefika mbele ya kitengo hicho kwa shughuli ya kuhojiwa siku za Jumatatu na Jumanne lakini wenzao zaidi waliongezwa kwenye orodha ya maafisa wanaochunguzwa. Waliamriwa wajitokeze kwa kuhojiwa kwa kina mwishoni mwa wiki huku wakitakiwa kufika pasi na kuwa na silaha yoyote.

Oktoba 20 wakati wa sherehe za Mashujaa, Rais Ruto alirejelea suala la SSU, akisema hakuna afisa wa polisi anayefaa kuhusika katika kifo au kutoweka kwa lazima kwa washukiwa.

Alitoa changamoto kwa polisi kuhakikisha usalama wa raia na kufanya kazi yao bila kuwaua washukiwa.

Raia hao wa India wanaaminika kualikwa nchini kusaidia chama cha siasa cha UDA katika maandalizi ya uchaguzi lakini walitoweka katika mazingira yasiyoeleweka.