Watumishi wa umma ambao walistaafu au kuondoka katika utumishi wa umma kwa njia moja au nyingine, sasa wana sababu ya kutabasamu baada ya Rais William Ruto kuamuru malimbikizi yote ya malipo ya uzeeni yalipwe katika muda wa miaka miwili.
Akihutubia mkutano wa wadau wa chama cha wadhamini wa malipo ya uzeeni na maafisa wa utawala nchini katika mtaa wa South C jijini Nairobi, Rais Ruto ameamuru wizara husika, idara na mashirika ya serikali kushirikiana na hazina za malipo ya uzeeni, vyama vya akiba na mikopo na taasisi nyingine za akiba na kuafikiana kuhusu mfumo wa kuhakikisha malimbikizi yote ya malipo ya uzeeni yamelipwa.
Amesema ni makosa kuchelewesha utoaji wa pesa hizo baada ya kukatwa kutoka kwa mishahara ya wanachama.
Rais alieleza kuwa utawala wake ulikuwa na nia ya kuweka kanuni ya kupatikana kwa ufadhili wa bei nafuu wa kiasi cha kutosha kufadhili miradi ya maendeleo kwa kiwango cha kuleta mabadiliko, na wakati huo huo kuunda. uwekezaji wa kuvutia.
"Lengo letu kuu ni kuunda ajira na kuboresha hali ya maisha ya mamilioni ya Wakenya wasio na uwezo," alisema.
Alibainisha kuwa mfumo unaofaa wa kisheria unapaswa kuwekwa ili kuboresha matarajio ya kustaafu na ustawi wa mamilioni ya wafanyakazi.
Hatua hiyo itakuwa afueni kwa watumishi wa umma waliostaafu ambao sasa wataweza kupokea malipo yao ya uzeeni kikamilifu katika muda wa miaka miwili ijayo.
Wakati huo huo, rais amekariri umuhimu wa kukuza mazoea ya kuweka akiba, akisisitiza kuwa serikali inalenga kudhibiti ukopaji wa pesa na kutumia akiba ya fedha za humu nchini kufadhili miradi ya maendeleo.