Rais William Ruto amesema kuwa Serikali ya Kenya Kwanza itaendelea kushirikiana na washirika wote katika kufanikisha usalama wa chakula na huduma ya afya kwa wote.
Ruto alifichua hayo alipokutana na mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates katika Ikulu ya Serikali, Jumatano.
Rais alitambua msaada unaotolewa na Bill & Melinda Gates Foundation nchini.
"Tunashukuru uungwaji mkono unaoendelea kutoa kwa Kenya katika kutimiza malengo yetu ya maendeleo, haswa katika nyanja za afya, kilimo na sekta ya ICT," Ruto alisema.
Gates ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku mbili aliwasili nchini Jumanne.
Ametembelea Makueni na alitazamiwa kutangaza dhamira ya kuunga mkono ubunifu mpya na werevu unaolenga kuboresha afya, usalama wa chakula na usawa wa kijinsia katika nchi za Afrika.