Msichana wa kuuza chakula ni miongoni mwa waliofariki katika mjengo ulioporomoka

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alidhibitisha hilo alipozuru Kasarani ambapo ghorofa hilo liliporomoka.

Muhtasari

• Tayari tumepata wale ambao wamefariki, kuna wale wa hapa, kuna msichana ambaye alikuwa anauza chakula na ni wa hapa Kasarani - Gavana Sakaja.

Jumba lililoporomoka Kasarani
Jumba lililoporomoka Kasarani

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja Jumatano alifanya ziara katika eneo la Kasarani ambapo mkasa wa jumba la ghorofa saba ulifanyika. Alikuwa ameandamana na diwani wa eneo hilo pamoja na mbunge wa Kasarani Ronald Karauri ambapo alitoa maelezo kuhusu watu ambao waliangamia kwenye mkasa huo.

Katika taarifa yake, Sakaja alielezea kwa huzuni mno kwamba mmoja wa walioangamia kwenye mjengo huo uliokuwa unaendelea ni msichana mmoja ambaye alikuwa anawauzia mafundi chakula.

Gavana alisema ni jambo la kusikitisha sana kwamba nchi inawapoteza watu nguvu kazi ya taifa kwa njia za kizembe kama hizo kwani jingo hilo halikuwa limepitishwa kujengwa na mamlaka ya kusimamia ujenzi NCA.

“Tayari tumepata wale ambao wamefariki, kuna wale wa hapa, kuna msichana ambaye alikuwa anauza chakula na ni wa hapa Kasarani, wengine ambao waliangamia ni kutoka maeneo mbali mbali Nairobi. Wote hawa waliamka asubuhi wakija kutafuta riziki yao, na wakapoteza maisha. Hili linasababishwa na ufisadi na kutojali,” Gavana alisema kwa hasira.

Alituma risala za rambirambi na kuahidi kwamab uongozi wake utatafuta njia ya kuwapa msaada familia zote za wale walioangamia kwenye vifusi vya jingo hilo ambalo mpaka wakati huo shughuli ya uokoaji ilikuwa imepamba moto.

“Tunatuma risala zetu za rambirambi na tutatafuta njia ya kutoa msaada wa wote walioathirika na kuporomoka kwa jingo hili. Lakini hili ni sharti liwe kama mfano wa mwisho kwa sababu najua kuna mijengo mingi inayoendelea pasi na kupitishwa na mamlaka husika,” Sakaja alisema.

Jingo hilo la ghorofa 7 liliporomoka Jumanne alasiri wakati ambapo ujenzi bado ulikuwa unaendelea na haijabainika kikamilifu idadi ya watu waliokwama kwenye vifusi vya jingo hilo.

Katika kuporomoka kwa jumba hilo mtaani Kasarani, shughuli za uokoaji zilianza mara moja ambapo mpaka mchana wa Jumatano, tayari miili ya watu 3 ilikuwa imetolewa kwenye vifusi vya jumba hilo. Watu 6 walikuwa wameokolewa.