Mwanamume apigwa risasi hadi kufa baada ya kutoa elfu 300 za kulipa mahari

Muhtasari
  • Inasemekana kuwa mwathiriwa alikuwa bado anapumua na nduguye alipofika eneo la tukio alikimbizwa katika hospitali ya karibu
Crime Scene
Image: HISANI

Huku visa vya uhalifu vikiongezeka nchini, na majambazi kukamatwa baadhi ya Wakenya bado wanaendelea kuathirika.

Kisa cha hivi karibuni ni cha mwanamume mwenye umri wa miaka 34, ambaye alipoteza maisha yake baada ya kupigwa risasi na watu wanaoaminikiwa kuwa majambazi siku ya Jumanne.

James Karanja, ambaye hadi kifo chake alikuwa mmiliki wa duka katika Makutano Shopping Centre, aliuawa kwa kupigwa risasi.

Inasemekana kuwa watu hao wanaoshukiwa kuwa majambazi walikuwa wakimfuatilia Karanja ambaye alikuwa katika harakati za kutayarisha mahari ya mkewe.

Alikuwa ametoka tu kutoa Ksh300,000 kutoka kwa benki, pesa zilizokusudiwa kulipa mahari ya mke wake huko Nyahururu katika sherehe iliyopangwa kufanyika Alhamisi, Novemba 17.

Hata hivyo, majambazi hao ambao walionekana kujiandaa vilivyo kwa ajili ya misheni hiyo waliruka pikipiki yao ya kuondoka kabla ya wananchi kufika eneo la tukio.

Wenyeji walimtahadharisha kakake marehemu ambaye alikuwa karibu na gari lake akingoja kuendelea na shughuli ya kuelekea Thika.

"Geuza gari lako! kaka yako amepigwa risasi lazima umkimbize hospitali!" ndugu huyo alisimulia alipokuwa akizungumza na Daily Nation.

Inasemekana kuwa mwathiriwa alikuwa bado anapumua na nduguye alipofika eneo la tukio alikimbizwa katika hospitali ya karibu.

Hata hivyo, alifariki kutokana na majeraha na kupoteza damu.

“Bado alikuwa akihema tulipofika hospitalini. Madaktari walimweka haraka kwenye mashine ya oksijeni na kuingiza bomba la IV kujaribu kukabiliana na upotezaji mkubwa wa maji. Kwa bahati mbaya haikufanya kazi na akafa,” kaka wa marehemu aliongeza.