Jengo lingine la ghorofa 5 laporomoka Ruiru, Kiambu

Hakuna aliyefariki au kujeruhiwa katika mkasa huo.

Muhtasari

• Hili ni jengo la 3 kuboromoka eneo la kiambu kufuatia lingine lililoporomoka eneo la Kiringiti, Ruaka na Ruiru sasa.

• Sasa tangu Wamatangi kuchukua hatamu ya uongozi nyumba 3 zimeboromoka

Hali halisi eneo la Ruiru baada ya jengo la ghorofa 5 kuporomoka
Hali halisi eneo la Ruiru baada ya jengo la ghorofa 5 kuporomoka
Image: AMOS NJAU

Visa vya majengo kuporomoka vinaendelea kushuhudiwa katika kaunti ya Kiambu huku jengo la hivi punde kuporoma likianguka mapema siku ya Jumatatu.

Jengo hilo lililokuwa mkabala na kituo cha polisi cha Ruiru liliripotiwa kuporomoka siku moja tu baada ya serikali ya kauti ya Kiambu kuwaamuru wakaazi waliokuwa wakiishi katika jengo hilo kuhama mara moja.

Hata hivyo kulingana na Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi  hakuna aliyefariki wala kujeruhiwa kkutokana na kisa hicho kwani kila mtu alikuwa ameagizwa kuhama. 

Siku ya Jumapili Wamatangi aliyekuwa amefika kwenye jengo hilo kusaidia katika shughuli ya kuwahamisha wakaazi, alisema jengo hilo lilikuwa dhaifu na lilikuwa na dalili kuwa ujenzi wake ulikuwa mbovu.

Alisema kuwa wakaazi wa jengo hilo walifaa kuhama ili utathmini wa ubora wake ufanyike kwanza.

"Hatutaruhusu mtu yeyote kuishi kwenye nyumba zilizojengwa vibaya kwani ni hatari, na nyumba hii ya Ruiru ni mojawapo," Wamatangi alisema.

Jengo hili la ghorofa 5 limeporomoka wiki moja tu baada ya jengo lingine la ghorofa 5 kuporomoka katika eneo la Ruaka Kiambu. Mkasa huo ulisababisha vifo vya watu watatu.

Miezi miwili iliyopita, watu 5 waliangamia katika eneo la Kirigiti na wengine 5 kujeruhiwa baada ya nyumba iliyokuwa ikijengwa kuporomoka.