Hamna tofauti yenu na magaidi,Kindiki awaambia wezi wa mifugo huku akiwaonya

“Wanaoiba mifugo na kuua watu hakuna tofauti kati yenu na magaidi,” alisema.

Muhtasari
  • Waziri huyo alisema kuwa majambazi hao wamewatia watu hofu kwa muda mrefu na hawakuadhibiwa lakini ni wakati wao wa kulipa
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI KITHURE KINDIKI
Image: KWA HISANI

Waziri wa Usalama wa Ndani amesema wameweka hatua kali kukabiliana na wezi wa mifugo huko Isiolo.

Akiongea na wakazi wa Isiolo siku ya Alhamisi, Kindiki alisema hataruhusu wezi hao kuwatisha watu na watasaka eneo hilo kwa makini hadi wawapate

"Ninataka kukuhakikishia kwamba tumepata habari kuhusu waliko na tunawatafuta," alisema.

"Tutawaadhibu na kuwachukulia hatua kwa sababu hakuna fisadi na mwizi, na hakuna jambazi ambaye ana nguvu za kutosha kuishinda serikali."

Kindiki alisema tayari wameanza kazi ya kuwatafuta na watawapata muda si mrefu.

“Tutawatafuta hao wezi, lazima tuhakikishe ulinzi unarudi na kwa majambazi siku zenu zinahesabika,” alisema.

Waziri huyo alisema kuwa majambazi hao wamewatia watu hofu kwa muda mrefu na hawakuadhibiwa lakini ni wakati wao wa kulipa.

“Wanaoiba mifugo na kuua watu hakuna tofauti kati yenu na magaidi,” alisema.