Washukiwa 16 wa ujambazi wakamatwa Embakasi

Polisi walisema kukamatwa kwa watu hao kulifanywa kwa haraka kufuatia malalamiko ya uporaji kutoka kwa umma

Muhtasari
  • Polisi walisema washukiwa wa uhalifu mbaya walinaswa Ijumaa usiku na kufungiwa katika kituo cha polisi cha Villa, kaunti ndogo ya Embakasi
Washukiwa 16 wa ujambazi wakamatwa Embakasi
Image: NPS/TWITTER

Washukiwa 16 wa ujambazi wamekamatwa Embakasi, Kaunti ya Nairobi.

Polisi walisema washukiwa wa uhalifu mbaya walinaswa Ijumaa usiku na kufungiwa katika kituo cha polisi cha Villa, kaunti ndogo ya Embakasi.

Watu hao walikamatwa saa 12.40 alfajiri na taarifa hizo zilitolewa katika kituo hicho.

Polisi walisema kukamatwa kwa watu hao kulifanywa kwa haraka kufuatia malalamiko ya uporaji kutoka kwa umma katika eneo la Transami na daraja la miguu.

"Maafisa wa polisi wakiandamana na timu ya NGAO walivamia maficho yaliyojengwa kwa miundo ya polythene na mabati na kukaliwa na familia za mitaani ndani ya TRANSAMI na kuwakamata wahalifu 16."

Polisi walisema walipokuwa wakipekua nyumba za kienyeji, bastola moja ya kuchezea, visu 37, panga 3, nyundo 2, makasi 6, masanduku 10 ya tokeni ya KPLC yanayoshukiwa kuibiwa, Roli 158 za bangi, gramu 500 za bangi, lita 2 za chang'aa, simu tatu za rununu na dekoda ya dijiti zilipatikana na kuwekwa kama maonyesho.

“Watashtakiwa kwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujitayarisha kufanya uhalifu,” polisi walisema.

Eneo hilo pia lilitembelewa na naibu kamishna wa kaunti na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo Embakasi.