KEMRI: Wakenya 23K hufa kila mwaka kutokana na kupika kwa kinyesi cha Wanyama

Pia kuna ushahidi unaoongezeka unaohusisha aina hii ya uchafuzi wa mazingira na kuzaliwa kwa watoto wenye uzito wa chini.

Muhtasari

• Takwimu zinaonyesha kuwa watu milioni 3.2 hufa kila mwaka kutokana na kuathiriwa na uchafuzi wa hewa wa kaya.

Image: Maktaba

Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya, KEMRI wiki jana ilitoa ripoti ambayo ni ya kutia huruma kwa maelfu ya Wakenya wanaofariki kutokana na kutumia nishati na kawi isiyofaa katika mapishi.

Kulingana na ripoti hiyo iliyochapishwa na majarida mbalimbali ya humu nchini, kila mwaka Wakenya takribani elfu 23 hufariki kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati kama vile mafuta ya taa, kuni, taka za mazao na kinyesi cha wanyama katika mapishi.

“Kupika kwa kutumia mafuta haya kumehesabiwa kuwa sawa na kuchoma sigara 100 kila saa, na hivyo kusababisha viwango vya HAP [uchafuzi wa hewa wa kaya] zaidi ya mara 100 viwango salama vya Shirika la Afya Ulimwenguni," Mkurugenzi Mkuu wa Kemri Prof Sam Kariuki alisema.

Pia kuna ushahidi unaoongezeka unaohusisha aina hii ya uchafuzi wa mazingira na kuzaliwa kwa watoto wenye uzito wa chini, TB, na magonjwa mengine mabaya, Prof Kariuki alisema.

Takwimu zinaonyesha kuwa watu milioni 3.2 hufa kila mwaka kutokana na kuathiriwa na uchafuzi wa hewa wa kaya, wakiwemo watoto 237,000 walio chini ya umri wa miaka mitano.

Katika Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa, watu 683,984 hufa kila mwaka kutokana na HAP, ikiwa ni asilimia 8.9 ya vifo vyote.

Theluthi moja ya watu duniani, takriban watu bilioni 2.4, hupika kwa kutumia moto wazi au majiko yasiyofaa yanayochochewa na mafuta ya taa, majani (kuni, mkaa, kinyesi cha wanyama na taka za mazao) na makaa ya mawe – ripoti hiyo ilisema.