Ripoti ya KHIS: Watoto wavulana zaidi ya 200 walilawitiwa Nairobi mwaka 2022 pekee

Ripoti hiyo ilisema kati yao, 121 ni wa chini ya miaka 11, huku 87 wakiwa kati ya miaka 12 hadi 17.

Muhtasari

• Viongozi sasa wametoa wito kwa jamii kuhusika kikamilifu ili kuzima visa hivi vya dhuluma kwa watoto.

Mwanaume aliyefungwa miaka 30 jela
Mwanaume aliyefungwa miaka 30 jela
Image: Mwananchi

Ripoti mpya ya serikali inasema kuwa watoto wa kiume wapatao zaidi ya 200 mwaka huu wa 2022 walilawitiwa jijini Nairobi pekee.

Kulingana na ripoti ya Mfumo wa Taarifa za Afya nchini (KHIS), wavulana 121 walio chini ya miaka 11 na wavulana 87 kati ya miaka 12 hadi 17 waliripotiwa kudhulumiwa kingono.

Jarida la Nation liliripoti kuwa Harriette Chiggai, Mshauri wa Rais kuhusu Haki za Wanawake, aliibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa visa vya GBV, kwa wanaume wa rika zote, wakati wa ziara yake katika Kituo cha Afya cha Mukuru, Nairobi Ijumaa iliyopita.

"Ulawiti katika nchi hii haizungumzwi kamwe lakini hatuwezi kunyamaza juu yake tena. Walioripotiwa hadi sasa Nairobi ni 208 tu, lakini idadi inaweza kuwa kubwa zaidi katika vijiji" Bi Chiggai alisema.

Pia alibainisha kuwa bado kuna visa vingi vya ukatili wa kijinsia ambavyo havijaripotiwa miongoni mwa wavulana.

Alibainisha kuwa mtoto wa kiume ameathiriwa sana na GBV lakini watu wanaombwa kutozungumzia hilo kwa sababu ‘ni kinyume na utamaduni wetu’, akieleza kuwa jambo hilo limemtenga mtoto wa kiume kupata msaada.

Viongozi wametoa wito kwa jamii kuingilia kati ili kutoa elimu na ushauri nasaha na pia kuchukua jukumu la kuripoti visa hivyo pindi vinapotokea kwa watoto wa kiume na pia wale wa kike.

“Jamii lazima ichukue jukumu la suala hili. Kwa muda mrefu, majirani walikuwa wazazi kwa kila mtoto katika jamii. Hata hivyo tumekuwa wabinafsi sana, unaona mtoto wa jirani yako anaumia na huchunguzi. Sote tunahitaji kuchukua jukumu la polisi. Tunaweza kusaidia serikali kutusaidia.”