Spika wa Seneti Amason Kingi amerejesha bunge kwa kikao maalum cha kujadili hoja ya kumtimua Gavana wa Meru Kawira Mwangaza ambayo ilipitishwa na Bunge la Kaunti ya Meru mnamo Jumatano, Desemba 14.
Kingi, kupitia notisi ya gazeti la serikali ya Desemba 16 alitangaza kwamba kikao hicho kinafuatia ombi la kiongozi wa wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na spika wa Bunge la Kaunti ya Meru Ayub Bundi kujadili suala hilo.
Kingi aliongeza kuwa kikao hicho kitafanyika katika mabunge makuu ya Seneti bungeni, kuanzia saa 2:30 jioni.
"Nimeteua Jumanne, tarehe 20 Desemba 2022 kama siku ya kikao maalum cha Seneti. ," ilisoma sehemu ya taarifa hiyo.
"Biashara itakayoendeshwa katika kikao hicho ni kusikilizwa kwa mashtaka dhidi ya Mhe. Kawira Mwangaza wa Kaunti ya Meru."
Mwangaza alitimuliwa baada ya MCAs 67 wa Meru kupiga kura kuunga mkono hoja yake ya kuondolewa madarakani ambayo ilipendekezwa kwa mara ya kwanza na MCA wa Abogeta Magharibi Dennis Kiogora, mnamo Novemba 22, 2022.