Mahakama ya Juu ilifanya uamuzi kulingana na ushahidi-Gavana Wamatangi kwa Azimio

"Mahakama ya Juu ilifanya uamuzi kulingana na ushahidi wote ambao ulitolewa mbele yake na pande zote mbili

Muhtasari
  • Aliwataka wanachama wa muungano wa Azimio kuzingatia kusimamia shughuli za serikali kama upinzani
GAVANA KIMANI WAMATANGI

Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi amepuuza ripoti ya Jumatano ya mtoa taarifa wa IEBC anayedai kuwa kiongozi wa Azimio La Umoja Raila Odinga alishinda Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Ripoti iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ilidai kuwa Raila alishinda kura baada ya kupata kura 8,170,355 mbele ya mshindani wake wa wakati huo na sasa rais, William Ruto, ambaye anadaiwa kupata kura 5,919,973.

Akizungumza siku ya  Alhamisi na runinga ya Citizen, Gavana Wamatangi hata hivyo alisema Mahakama ya Juu tayari ilikubali ushindi wa Ruto na nchi inahitaji kuendelea na mbele.

"Mahakama ya Juu ilifanya uamuzi kulingana na ushahidi wote ambao ulitolewa mbele yake na pande zote mbili na walithibitisha kwamba ushindi uliotangazwa huko Bomas ulikuwa ni mapenzi ya watu wa Kenya," gavana huyo mshirika wa UDA alisema.

Aliwataka wanachama wa muungano wa Azimio kuzingatia kusimamia shughuli za serikali kama upinzani, badala ya kile alichoeleza kuwa ni kurusha vibao katika kazi ya serikali ya Kenya Kwanza.

"Hadithi hizi zote kuhusu makabrasha ndizo zinazotokea mara nyingi unapokuwa na mtu aliyeshindwa katika uchaguzi, kwa bahati mbaya. Mara tu unaposhindwa kwa haki, fanya kazi na utulie…Raila Odinga anafaa kuiacha serikali ifanye kazi, kuongoza upinzani na kufanya kazi ya uangalizi,” alisema Wamatangi.