Msichana aokolewa baada ya kuozwa na mama yake kwa shillingi elfu tatu

Muhtasari
  • Oula alisema mama ya msichana huyo alikiri kwamba hivi majuzi raia huyo wa Uganda alimpa Ksh.3000 kama mtaji wa kuanzisha biashara
Mtahiniwa mjamzito
Mtahiniwa mjamzito
Image: Maktaba

Msichana aliyefanya mtihani wa Cheti cha Elimu ya Msingi nchini (KCPE) katika shule ya msingi ya Osiri katika Kaunti Ndogo ya Nyatike kaunti ya Migori na kupata alama 135 ameokolewa kutoka kwa ndoa ya mapema.

Chifu wa  Mikeyo David Oula alisema walimuokoa msichana huyo ambaye amekuwa akiishi na raia wa Uganda, mwenye umri wa miaka 40, anayesemekana kufanya kazi ya kawaida katika eneo hilo.

Bw Oula alisema wazazi wa msichana huyo walikiri kumuoza msichana wao  akisisitiza kwamba binti yao ambaye alifanya mtihani wa KCPE 2022 na hana akili timamu ana umri wa miaka 22 na hivyo si mtoto mdogo.

Oula alisema mama ya msichana huyo alikiri kwamba hivi majuzi raia huyo wa Uganda alimpa Ksh.3000 kama mtaji wa kuanzisha biashara kabla ya kumwachilia msichana huyo.

Alisema uchunguzi wao wa awali umebaini kuwa raia huyo wa Uganda ambaye anafanya kazi ya kuchimba dhahabu amekuwa kwenye mapenzi ya lazima na msichana huyo tangu akiwa darasa la sita na familia ya wazazi hao imekuwa ikipokea msaada wa fedha kwa kubadilishana.

Chifu wa eneo hilo alisema msichana huyo alifichua kwamba amekuwa akitamani kuendelea na masomo yake katika shule ya upili lakini wazazi wakasisitiza kwamba lazima aolewe na mwanamume huyo.

Bw Oula alisema walikuja kumuokoa msichana huyo kufuatia simu zilizoendelea kutoka kwa majirani waliodai msichana huyo amekuwa akilia mchana na usiku akimsihi mwanamume huyo wa Uganda amrudishe kwa wazazi wake ili aendelee na masomo.

Haya yanajiri siku chache baada ya mzee mmoja kufungwa kifungo cha maisha kwa kumuoa msichana wa miaka 9.