"Imekuwa pigo kubwa kwa familia" Moses Kuria atoa heshima ya mwisho kwa dadake mkubwa

"Saratani imeiba kama mtu mwenye bidii na aliyejitolea," Kuria alisema.

Muhtasari

•Nyokabi alifariki mnamo Januari 13 katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta baada ya kupambana na saratani kwa muda.

•Kuria alitoa shukrani za dhati kwa rais na naibu yake kwa kushirikiana na familia yao katika kumzika dada yake.

wakati wa mazishi ya dadake mkubwa, Pauline Nyokabi.
Waziri wa Biashara Moses Kuria wakati wa mazishi ya dadake mkubwa, Pauline Nyokabi.
Image: PCS

Dada mkubwa wa Waziri wa Biashara Moses Kuria, marehemu Pauline Nyokabi Kuria hatimaye alizikwa siku ya Jumatatu.

Nyokabi alifariki mnamo Januari 13 katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta baada ya kupambana na saratani kwa muda.

Alizikwa nyumbani kwake katika eneo la Gatundu Kusini katika hafla iliyopambwa na viongozi wakuu wa kitaifa wakiwemo Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.

Akizungumza baada ya mazishi, Kuria alibainisha kuwa kumpoteza dadake mkubwa ambaye walimtambua kama "Naibu Mama" kumekuwa pigo kubwa kwa familia.

"Kupoteza mpendwa si rahisi. Kumpoteza dada yetu mkubwa imekuwa pigo kubwa sana kwa familia yetu kwa kuwa tulikua tunamfahamu kama "naibu mama" wetu. Saratani imeiba kama mtu mwenye bidii na aliyejitolea," Alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha kadhaa za hafla hiyo iliyohudhuriwa na wanafamilia, viongozi na watu wengine wa karibu.

Kuria alichukua fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa rais na naibu yake kwa kushirikiana na familia yao katika kumzika dada yake.

"Kwa mawaziri wenzangu, asanteni sana kwa kuomboleza pamoja na familia yangu na kufika nyumbani kwetu tulipokuwa tukisherehekea maisha ya dada yetu Pauline.

Siwezi kusahau kuwashukuru viongozi wote wa kisiasa waliojitokeza kwa ajili yetu. Asanteni kwa kumkumbuka aliyekuwa mwenzenu na familia yake katika nyakati hizi za majaribu," aliandika waziri huyo.

Mbunge huyo wa zamani wa Gatundu Kusini pia aliwashukuru Wakenya kwa kusimama naye na kumfariji wakati wa majonzi.

"Pauline, dada yetu, pumzika kwa amani," alisema.

Viongozi waliohudhuria mazishi ya Nyokabi ni pamoja na Rais William Ruto, Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri Kipchumba Murkomen, Gavana Anne Waiguru, Senetor Karungo Thangwa miongoni mwa wengine.