Siko tayari kumwapisha Raila tena-Miguna aweka wazi

Miguna pia alisema hayuko tayari kuwasaidia viongozi wa upinzani kuwarai wafuasi wao kutomtambua William Ruto kama Rais halali wa Kenya.

Muhtasari
  • Aidha alimshutumu Raila kwa ulaghai, akisisitiza kuwa wakati huu, Waziri Mkuu huyo wa zamani yuko peke yake
Image: TWITTER// MIGUNA MIGUNA

Wakili Miguna Miguna amesema hatapatikana ili kumuapisha Raila Odinga kama 'Rais wa Wananchi' kwa mara ya pili.

Miguna pia alisema hayuko tayari kuwasaidia viongozi wa upinzani kuwarai wafuasi wao kutomtambua William Ruto kama Rais halali wa Kenya.

Aidha alimshutumu Raila kwa ulaghai, akisisitiza kuwa wakati huu, Waziri Mkuu huyo wa zamani yuko peke yake.

"Tafadhali mwambie @RailaOdinga  Mkuu @MigunaMiguna hapatikani kumwapisha kama Rais wa Wananchi, wala siko tayari kumsaidia kugomea au kumpinga Rais ALIYECHAGULIWA HALALI wa Jamhuri ya Kenya. Yule mwoga na msaliti yuko peke yake!"

Matamshi ya Miguna yanajiri siku chache baada ya  tangazo la Raila wakati wa mkutano wa Kamukunji Jumatatu kwamba Ruto aliiba kura ya urais ya Agosti 9, 2022.

"Hatutambui utawala wa Kenya Kwanza kama serikali halali na Ruto kama rais au afisa yeyote katika serikali yake," Raila alisema.