Huduma kidijitali: Shirika la reli nchini lapiga marufuku pesa taslimu katika kununua tikiti

Shirika hilo lilisema agizo hilo linaanza kufanya kazi Februari mosi katika vituo vyote vya treni za Madaraka Express.

Muhtasari

• "Hivyo basi wateja wanaombwa kutumia mifumo ya M-Pesa au kadi za benki katika vituo vyote,” - Kenya Railways walisema.

Mamlaka ya Keli ya Kenya
Mamlaka ya Keli ya Kenya
Image: Image: picha:twitter /Hisani

Shirika la reli nchini limetangaza kukumbatia mfumo wa kidijitali wa kulipia tikiti za usafiri katika usafiri wa treni za Madaraka Express.

Agizo hilo la kupiga marufuku ulipaji wa pesa taslimu lilianza kutekelezwa Februari mosi ambapo wasafiri wote wameombwa kukumbatia mfumo wa kidijitali wa kununua tikiti kutumia M-Pesa.

“Tungependa kuwataarifu wateja wetu na umma wote kwa jumla kwamba kuanzia Februari mosi, 2023, hatutakuwa tunakubali malipo kwa ajili ya tikiti kupitia pesa taslimu katika vituo vyote vya treni za Madaraka Express kote nchini. Hivyo basi wateja wanaombwa kutumia mifumo ya M-Pesa au kadi za benki katika vituo vyote,” taarifa hiyo fupi ilisoma kwa ukamilifu.

Uhamiaji huu kutoka mifumo ya zamani hadi mifumo ya kisasa ya kidijitali ni moja ya ajenda kubwa katika serikali ya rais William Ruto, ambaye amekuwa akisema kwamba huduma nyingi katika ofisi za serikali zitakuwa zikitolewa kwa njia za kidijitali.

Hapo jana, rais aliongoza kikao cha baraza la mawaziri wake cha kwanza ambacho kilikuwa bila matumizi ya kalamu na karatasi, kwani waliohudhuria wote walionekana wakitumia vishkwambi na talakilishi.

Hiyo jana pia, serikali ilitangaza kwanzia mwezi Machi mwaka huu, vyeti vya kuzaliwa na vyqa kufa vyote vitakuwa vinatolewa kwa njia za kidijitali.

Katibu Mkuu wa Uhamiaji na Huduma kwa Raia Julius Bitok alisema IPU itatumika kama nambari ya shule za msingi na shule za upili, nambari ya Kitambulisho cha Kitaifa, Nambari ya KRA, nambari ya leseni ya kuendesha gari, na mtu akifa, atatambuliwa moja kwa moja na nambari hiyo.

"Serikali inasogeza huduma mtandaoni kufikia Machi, na vyeti vyote vya kifo na kuzaliwa vitakuwa mtandaoni," Bitok alisema.