Raila amwomba Kingi aruhusu Azimio kufanya mabadiliko ya uongozi katika Seneti

Pamoja naye walikuwa maseneta Ledama Ole Kina (Narok), Enock Wambua (Kitui) na Edwin Sifuna (Nairobi).

Muhtasari
  • Alisisitiza kuwa vyama vya siasa viruhusiwe kufanya mabadiliko ya uongozi wao ndani ya Bunge bila kuingiliwa
KINARA WA AZIMIO RAILA ODINGA
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga amemtaka Spika wa Seneti Amason Kingi kuruhusu upande wa Wachache kuwa na uongozi unaotaka katika Bunge.

Akizungumza na vyombo vya habari katika majengo ya Bunge, Raila alisema Kingi anafaa kuwaachia upinzani kuwa na uongozi unaotaka katika Bunge hilo.

“Tuna changamoto za uongozi katika Seneti. Uongozi wa vyama vya siasa usiingiliwe,” alisema.

Alishangaa ni kwa nini Kingi bado hajafanya mabadiliko katika Seneti licha ya Azimio kupata viongozi wapya katika Bunge hilo.

Alisisitiza kuwa vyama vya siasa viruhusiwe kufanya mabadiliko ya uongozi wao ndani ya Bunge bila kuingiliwa.

“Chama cha siasa kinapofanya mabadiliko yake, hakipaswi kuingiliwa. Tunamwomba Spika au mtu mwingine yeyote kuruhusu Azimio la Umoja-One Kenya Alliance kufanya mabadiliko katika uongozi wake wapendavyo,” akasema.

Pamoja naye walikuwa maseneta Ledama Ole Kina (Narok), Enock Wambua (Kitui) na Edwin Sifuna (Nairobi).

Raila aliteta kuwa Bunge halina shughuli ya kutumbuiza maagizo ya mahakama.

Fatuma Dullo (Isiolo) ambaye alikuwa ameteuliwa kung’olewa kwenye nafasi ya Mnadhimu wa Walio wachache alihamia Mahakama ya Mizozo ya Vyama vya Siasa (PPDT) akipinga uamuzi wa Azimio kumwondoa katika nafasi hiyo.

Maandamano ya Raila yanakuja baada ya Kingi kukosa kutangaza mabadiliko ya uongozi katika Bunge.