Pasta akamatwa baada ya mwanamke aliyekuwa wakikutana kwa ajili ya 'maombi' kupatikana amekufa Ruiru

Alikuwa ameenda mafichoni tangu Februari 8, 2023, baada ya kudaiwa kumuua Christine Makena Maingi.

Muhtasari
  • Hata hivyo, uchunguzi wa maiti uliofanywa kwenye mwili wa marehemu ulionyesha kuwa alikufa kutokana na kunyongwa na kuondoa uvumi wa kujitoa mhanga
Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika eneo la Ruiru Kaunti ya Kiambu wanamshikilia mshukiwa kuhusiana na mauaji ya mwanamke mwenye umri wa miaka 35 mwezi uliopita.

KUlingana na ripoti za Citizen Digital Christopher Kiptum Keter mwenye umri wa miaka 50 aliondolewa katika maficho yake katika mtaa wa mabanda wa Mukuru kwa Njenga wa Embakasi mnamo Jumanne, Machi 7.

Alikuwa ameenda mafichoni tangu Februari 8, 2023, baada ya kudaiwa kumuua Christine Makena Maingi.

Kulingana na ripoti za polisi, Kiptum ambaye anaaminika kuwa mchungaji ndiye mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu.

Picha za CCTV na mawasiliano ya simu za rununu zilizopatikana na wapelelezi zilifichua kuwa wawili hao walikuwa pamoja usiku wa Februari 5 na 6 kabla ya mwili wa Makena uliokuwa ukiharibika kugunduliwa siku mbili baadaye katika jumba la makazi eneo la Gathogora ndani ya Kaunti Ndogo ya Ruiru.

Katika eneo la uhalifu, dawa pia zilipatikana na kuwapa wachunguzi hisia ya awali kwamba marehemu alijiua kwa kutumia dawa  kupita kiasi.

Hata hivyo, uchunguzi wa maiti uliofanywa kwenye mwili wa marehemu ulionyesha kuwa alikufa kutokana na kunyongwa na kuondoa uvumi wa kujitoa mhanga.

Taarifa za polisi zinaendelea kusema kuwa mshukiwa na marehemu walikutana mara kwa mara nyumbani kwa marehemu alikokuwa akiishi na wazazi wake.

Wakati kisa hicho kilipotokea, wanafamilia hao walikuwa wamesafiri.

Wanafamilia wanasema Makena alimtambulisha mshukiwa kama mchungaji na wangekutana mara kwa mara kwa vipindi vya maombi.

Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza katika safari ya kutoka Mombasa hadi Nairobi mapema mwaka huu.

Mshukiwa yuko chini ya ulinzi wa polisi akisubiri kufikishwa mahakamani siku ya Alhamisi kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 203 cha kanuni ya adhabu.