Meru: Wafanyikazi wa kaunti kushiriki ibada ya maombi mara tatu kwa wiki

Nyimbo za sifa na ibada zitaanza 6:45AM hadi 7AM, maombi yatachukua dakika 15 kutoka hapo na mahubiri kuanza 7:15AM hadi 7:30AM.

Muhtasari

• Maombi hayo yatakuwa yanafanyika mara tatu kwa wiki, Jumatatu, Jumatano na Ijumaa katika chumba cha mikutano cha kaunti hiyo.

Gavana wa Meru akiombewa
Gavana wa Meru akiombewa
Image: Facebook

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza ametangaza ratiba mpya ya maombi kwa wafanyikazi wote wa kaunti hiyo ambayo itaanza kutekelezwa kuanzia Jumatatu tarehe 13, ambayo ni leo.

Kupitia bango ambalo gavana huyo aliyenusurika kutimuliwa madarakani alipakia kwenye ukurasa wake wa Facebook, sasa ni rasmi kwamba wafanyikazi wote wa kaunti walashiriki ibada ya maombi kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kila wiki.

Kulingana na ratiba hiyo, ibada ya maombi itakuwa inafanyika katika chumba cha mikutano cha kaunti hiyo na kuanzia saa moja kasoro robo hadi saa moja kamili asubuhi, itakuwa ni nyimbo za sifa na ibada.

Saa Moja kamili hadi saa moja na robo ni maombi yatakayokuwa yakiongozwa huku kuanzia saa moja na robo hadi saa moja na nusu itakuwa ni mahubiri.

Taarifa hii inakuja siku chache tu baada ya taarifa nyingize ambazo hata hivyo hazikudhibitishwa kutoka ikulu kwamba rais Ruto amewaagiza wafanyikazi wa ikulu kushiriki maombi katika siku teule za wiki.

Baadhi ya watu waliotoa maoni yao katika tangazo hilo la gavana Mwangaza walimtaka hata hivyo asiweke shuruti kwa ratiba hiyo na maombi yawe ni jambo la kujitolea tu kwa wafanyikazi.

“Ilimradi haufanyi kuwa jambo la lazima. Usianze kugombana na wafanyikazi wa kaunti wanaokosa vipindi hivyo vya maombi. Kila Mkenya ana uhuru wa kuabudu. Wanaweza kuchagua kuwa wa madhehebu ya kidini unayojiandikisha, au wanaweza kuchagua kutoshiriki,” Lewis Kithinji Mugambi alisema.

Wengine walimpongeza kwa hilo wakisema kwamba ndio uamuzi wa njia sahihi kutanguliza maombi katika kila hatua.

“Mheshimiwa Gavana Mh Kawira Mwangaza kwa maombi kila kitu kinawezekana tunaamini... Lakini Gavana wangu wa Kaunti ya Meru sisi wa imani tofauti tunafikiria kuwaalika wengine,” mwingine alisema.