Mtoto wa miaka 2 aliyetoweka Machakos apatikana Kakamega

Mtoto huyo wa kiume alisafirishwa kwa utata hadi Kakamega na kuachwa karibu na boma moja mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Muhtasari

• Wakazi baada ya kupata mtoto huyo, walipiga ripoti rasmi kwa polisi na kukabidhiwa idhini ya kuishi naye kwa muda.

• Ripoti hiyo ilipeperushwa runingani na baba mzazi akafululiza kutoka Mlolongo hadi Kakamega kujumuika na mwanawe.

Mtoto aliyetoweka Mlolongo apatikana Kakamega
Mtoto aliyetoweka Mlolongo apatikana Kakamega
Image: Screengrab//Citizen TV

Mtoto wa miaka miwili aliyeripotiwa kutoweka kutoka nyumbani kwao Mlolongo kaunti ya Machakos mwishoni mwa juma lililopita hatimaye amepatikana katika kaunti ya Kakamega na kujumuishwa na familia yake.

Kulingana na ripoti iliyopeperushwa katika runinga ya Citizen wikendi iliyopita, Andrew Kinyua, mtoto wa kiume wa miaka miwili alipatikana katika boma moja Matungu kaunti ya Kakamega ambako aliripotiwa kuachwa Jumamosi jioni na mtu asiyejulikana.

Wakaazi wa mtaa mmoja katika kaunti ya Kakamega walieleza kwamba walimshuhudia mwanamke asiyetambulika akifika hapo mwendo was aa kumi na mbili jioni na kumuacha mtoto huyo pale kabla ya kuondoka bila taarifa.

Mmoja wa wanawake hao ambao walikuwa wa kwanza kumuona mtoto yule alieleza kwamab baada ya kumaliza shughuli zake, aliona mtoto akimpungia mkono na moja kwa moja silika yake ikamtuma kwamba huenda ni mumewe ameletewa mtoto aliyekuwa amezaa nje ya ndoa.

"Baada ya kumaliza kazi yangu, niliona mtoto akipunga mkono na kwenda kumkabili mume wangu kama alikuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na mtu ambaye alikuja kumwacha mtoto karibu naye," Okello alisema mume wake alikanusha kuwa na uhusiano nje ya ndoa.

Wanandoa hao kisha walitoa ripoti rasmi katika kituo cha polisi cha Koyonzo, ambapo walipewa haki ya kumlea kwa muda mvulana huyo wa miaka miwili hadi Jumatatu, ambapo hatua zaidi zingechukuliwa.

Hata hivyo, ripoti iliyowasilishwa na runinga ya Citizen siku ya Jumamosi ilimjulisha Boniface aliko mwanawe, na akafunga safari hadi Koyonzo huko Mumias, ambapo baada ya kuhojiwa kwa saa tatu, Kinyua aliunganishwa tena na mwanawe.