Tafadhali mwite Raila muongee-Mbunge wa Mavoko Makau amsihi Ruto

Pia amemtaka Rais Ruto kutekeleza sera alizowaeleza Wakenya kwenye manifesto yake alipokuwa akiwania kiti hicho.

Muhtasari
  • Mbunge huyo wa chama cha Wiper lilimkashifu Rais William Ruto kwa kulaumu utawala wa Uhuru Kenyatta kwa matatizo ya kiuchumi
MBUNGE WA MAVOKO PATRICK MAKAU

Mbunge wa Mavoko Patrick Makau amemtaka Rais William Ruto kuwasiliana na kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga na kufanya mazungumzo kuhusu gharama ya juu ya maisha.

Akizungumza huko Kyumbi, Kaunti ya Machakos alipokuwa akiwagawia wanafunzi basari, mbunge wa Mavoko Makau alisema ni lazima viongozi hao wawili sasa wakae  na kuafikiana jinsi watakavyopunguza gharama ya maisha na kupunguza mzigo wa kiuchumi ambao Wakenya wanakabili kwa sasa.

“Na mimi nauliza Ruto, tafadhali ita Raila mkae chini muangalie hii maneno ya uchumi wa Kenya. Ukikaa tu hivi ukimuita mganga, rafiki yangu utaumia,” alisema.

Mbunge huyo wa chama cha Wiper lilimkashifu Rais William Ruto kwa kulaumu utawala wa Uhuru Kenyatta kwa matatizo ya kiuchumi ambayo yameikumba nchi ikisema ujenzi wa uchumi hauhitaji maonyesho, kupiga kifua na kutaja majina.

“Uchumi wa Kenya hautajengwa kwa maonyesho ya kando, kutaja majina, na kupiga kifua. Uhuru Kenyatta alifanya miaka kumi na akastaafu. Usimburute kwenye fujo hii,” anasema.

Pia amemtaka Rais Ruto kutekeleza sera alizowaeleza Wakenya kwenye manifesto yake alipokuwa akiwania kiti hicho.

“Tuonyeshe ni wapi utatupeleka kama Wakenya na mwongozo wako wa kiuchumi. Acha kusema rasilimali ziliporwa na utawala uliopita,” Alizungumza.