Rais Ruto amuonya Raila Odinga dhidi ya maandamano yenye vurugu

Rais alisema Kenya ni nchi inayoongozwa kwa sheria na hakuna aliye juu ya sheria.

Muhtasari

•Rais William Ruto alisisitiza kwamba hataruhusu jaribio lolote la Odinga kusababisha machafuko nchini.

•Rais Ruto aliambia kiongozi wa upinzani kuwa nchi haitasalimu amri kwa vitisho na 'ulaghai' wake.

Rais William Ruto amemtahadharisha kiongozi wa upinzani Raila Odinga dhidi ya kufanya maandamano haramu yatakayosababisha vifo, uharibifu wa mali au kulemazwa kwa shughuli za biashara nchini.

Huku akijibu vitisho vya hivi majuzi vya Odinga na viongozi wengine wa upinzani vya kuongoza maandamano ya nchi nzima wiki ijayo, Rais alisema Kenya ni nchi inayoongozwa kwa sheria na hakuna aliye juu ya sheria.

Rais alisisitiza kwamba hataruhusu jaribio lolote la Odinga kusababisha machafuko nchini, akimtaka kuwasiliana na polisi kuhusu maandamano yaliyopangwa.

"Lazima tumwambie rafiki yangu Raila Odinga.  Huwezi kuendelea kuhujumu nchi. Hatuna shida na wewe kuandaa maandamano lakini tafadhali ni jukumu lako kushirikiana na polisi kuhakikisha kuwa maisha ya raia wengine hayavurugwi na mali zao haziharibiwi wala biashara kasimamishwa .Wanaweza kwenda kazini na wewe endelea na maandamano yako."

Rais alikuwa akizungumza katika Ikulu ya Nairobi, Jumatano, alipokutana na viongozi kutoka Kaunti ya Trans Nzoia. Alisema Wakenya wana haki ya kuandamana lakini lazima wafanye hivyo kwa amani na kwa mujibu wa sheria.

 "Tunamwambia Bw. Raila, tafadhali tupe heshima kidogo. Hata sisi ni Wakenya. Si wewe peke yako Mkenya."

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Naibu Rais Rigathi Gachagua, Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula, Katibu wa Baraza la Mawaziri Susan Nakumicha na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya. Wengine walikuwa wabunge Lilian Siyoi (Mwakilishi wa Wanawake), Patrick Barasa (Cherangani), Allan Chesang (Trans Nzoia), Ferdinand Wanyonyi (Kwanza) na waliokuwa wabunge Joash Wamangoli na Noah Wekesa miongoni mwa wengine.

Rais Ruto aliambia kiongozi wa upinzani kuwa nchi haitasalimu amri kwa vitisho na 'ulaghai wake.' “Nataka kumwambia kaka yangu mkubwa Raila Odinga kwamba hatuwezi kuwa na seti mbili za sheria,” alisema Dkt Ruto.

Naibu rais Gachagua aliwapongeza viongozi hao kwa azimio lao la kufanya kazi na serikali kwa ajili ya maendeleo. "Nina furaha kwamba wewe si sehemu ya wanaopanga maandamano. Kwa nini Raila Odinga hakuandamana wakati gharama ya mbolea ilikuwa Sh 7,000 na bei ya unga Sh 250?' Bw Gachagua alihoji.

Bw Mudavadi alimkashifu Bw Odinga kwa kutoa matamshi ya uwongo ambayo hayana msingi wa kisheria. "Tuko katika nchi ambayo inaongozwa na sheria. Ni makosa kwa mtu yeyote kutangaza sikukuu ya umma kwa kupuuza utawala wa sheria," alisema Bw Mudavadi. Acha maoni