Wadau wa elimu wataka serikali kuahirisha siku ya wanafunzi kurejea shuleni

•Raila aliitisha maandamano tarehe 20 Jumatatu

Muhtasari

•Kinara wa Azimio, Raila Odinga alitangaza kuwepo kwa maandamano ya kitaifa siku ya jumatatu tarehe ishirini.

Makatibu wa vyama vya walimu KUPPET na KNUT
Makatibu wa vyama vya walimu KUPPET na KNUT
Image: TWITTER

Wazazi na walimu wameelezea wasiwasi wao kuhusu usalama wa wanafunzi siku ya Jumatatu wanapotarajiwa kuripoti kutoka kwa likizo fupi kutokana na maandamano ya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Wanafunzi walianza mapumziko yao ya katikati mwa muhula na wameratibiwa kurejea Jumatatu siku ambayo Azimio itafanya maandamno.

Kutokana na hali hii mwenyekiti wa muungano wa wazazi nchini Silas Obuhatsa alitoa wito kwa aliwasihi Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio Raila Odinga kufanya mazungumzo ili kuepusha taifa mgogoro wa kisiasa.

"Kwa maandamano, huwezi kamwe kujua matokeo. Kuna wazazi wanaounga mkono miungano ya Azimio na Kenya Kwanza. Tunatoa wito kwa viongozi hao wawili kufanya mazungumzo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya watoto ambao hawana hatia. Watoto hawakupiga kura,” Obuhatsa alisema.

 

Bw Obuhatsa alielezea hofu kuwa huenda usafiri wa kuelekea maeneo mbalimbali nchini ukaathiriwa siku ya Jumatatu, huku wanafunzi wanaolazimika kusafiri umbali mrefu wakitatizika. 

"Baadhi ya wahuni wanaweza pia kuchukua fursa ya hali hiyo kuwadhuru watoto. Katika hali kama hiyo, wangependa kuwa na wazazi wao,” Bw Obuhatsa alisema.

Mwenyekiti wa Muungano wa Kuppet Omboko Milemba alitoa wito wa kuahirishwa kwa siku ya kurejea shuleni hadi Jumatano ili kuwaepusha na machafuko ya maandamano.